Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Hemed Said Magaro ameongoza Timu ya Menejimenti ya Halmshauri ya wilaya ya Kilwa (CMT) kufanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Njinjo, Mitole na Kikole Wilayani Kilwa kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wananchi kwa kutoa huduma bora. Ziara hiyo imefanyika tarehe 22/02/2025.
Katika ziara hiyo Timu ya Menejimenti imekagua mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Njinjo wenye thamani ya Tsh. 52,000,000/= fedha kutoka mapato ya ndani, ujenzi wa Mnada wa Mifugo wa kijiji cha Njinjo wenye thamani ya Tsh. 50,000,000/= fedha kutoka mapato ya ndani, Ukarabati wa Shule ya Msingi Kipindimbi wenye thamani ya Tsh. 101,000,000/= fedha kutoka kwa wafadhili kupitia mradi wa BOOST, Umaliziaji wa darasa moja katika shule ya Msingi Kipindimbi wenye thamani ya Tsh. 22,459,365/= fedha kutoka mapato ya ndani, na Umaliziaji wa madarasa mawili Shule ya Msingi Njinjo wenye thamani ya Tsh. 15,000,000/= fedha kutoka mapato ya Ndani.
Aidha Timu ya Menejimenti imekagua mradi wa ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Ndende iliyoko katika Kata ya Mitole wenye thamani ya Tsh. 68,000,000/= ambapo kiasi cha Tsh. 20,000,000/= ni fedha kutoka Mfuko wa Elimu na kiasi cha Tsh. 48,000,000/= ni fedha kutoka mapato ya ndani. Pia ukaguzi umefanyika katika Ujenzi wa matundu kumi ya vyoo katika Shule ya Msingi Mitole wenye thamani ya Tsh. 11,000,000/- fedha kutoka mapato ya ndani, Umaliziaji wa maabara katika Shule ya Sekondari Kikole wenye thamani ya Tsh. 6,000,000/= fedha kutoka Mfuko wa Jimbo na ujenzi wa matundu kumi ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kikole wenye thamani ya Tsh. 11,000,000/= fedha kutoka mapato ya Ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji amewapongeza wataalamu wanaosimamia ujenzi wa miradi hiyo lakini pia amewataka kuongeza juhudi katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili ilete manufaa kwa wananchi. Sambamba na hilo Ndg. Magaro amesisitiza kuzingatia Thamani ya fedha na ubora wa mradi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi hiyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa