Kamati mbalimbali za maandalizi ya Sherehe za Majimaji katika Wilaya ya Kilwa zimekutana kufanya kikao kazi maalum chenye lengo la kuratibu na kujadili hatua muhimu kuelekea sherehe za Majimaji na urithi wa Kilwa zinazotarajiwa kuvuta hisia za wakazi na wageni kutoka maeneo mbalimbali.
Kikao hicho kimefanyika Tarehe 13 Agosti 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho Mhe. Mohamed Nyundo ametilia mkazo suala la ushirikiano miongoni mwa wanakamati wote, huku akisisitiza mafanikio ya sherehe hizo yatategemea kwa kiasi kikubwa mshikamano na utendaji wa pamoja.
Kikao hicho pia kimejadili mambo kadhaa muhimu yakiwemo maandalizi ya miundombinu, burudani, ushiriki wa wanakijiji, pamoja na uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo kushiriki kupitia sherehe hizo.
Wanakamati wameahidi kushirikiana kwa karibu kuhakikisha kila kamati inatekeleza wajibu wake kwa wakati, ili Sherehe za Majimaji za mwaka huu ziwe za kipekee na zenye mafanikio makubwa zaidi kuliko miaka iliyopita.
Sherehe hizo, ambazo huadhimisha kumbukumbu ya mapambano ya kihistoria ya Majimaji dhidi ya ukoloni, ni tukio muhimu katika kalenda ya Wilaya ya Kilwa na huwaleta pamoja wanajamii kutoka sehemu mbalimbali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa