District Medical Officer(DMO)
IDARA YA AFYA
Utangulizi.
Huduma za Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa hutolewa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wengine kwa maana ya watu na mashirika binafsi (Public Private Partnership) chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa zikisimamiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri.
VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.
Huduma ya Afya Wilayani hutolewa katika ngazi mbalimbali za matibabu katika jumla ya Vituo 55, Hospitali 2, moja ya Serikali (Hospitali ya Wilaya) na nyingine ya Shirika la Dini (Hospitali ya Kipatimu) ambayo vilevile hutoa huduma kwa mkataba na Halmashauri ya Wilaya kwa watoto na Mama wajawazito (Service Agreement), Vituo vya Afya 5 vya serikali, Zahanati 48 kati ya hizo Zahanati 1 ni ya Shirika la dini na 1 ni ya binafsi. Zahanati 14 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
HALI YA WATUMISHI WA KADA ZA AFYA WILAYANI
Halmasshauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya watumishi 335 wa kada mbalimbali za Afya (sawa 25%) kati ya 1315 wanaohitajika kukidhi ikama ya watumishi kwa mujibu wa Mwongozo wa Ikama wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (2014-2019). Kati ya watumishi waliopo 335, Watumishi wenye ujuzi (Skilled Personal) ni 158 sawa na 47%. Watumishi 177 ni wale wasio na ujuzi (Unskilled personnel) sawa na asilimia 53%. Aidha athari ya upungufu wa watumishi huonekana sana katika ngazi za chini za vituo vya huduma hususani Zahanati ambako vituo vingi vina watumishi aidha mmoja au wawili.
MAJUKUMU YA IDARA
JITIHADA ZINAZOCHUKULIWA KATIKA KUPAMBANA NA UKIMWI
Mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI yanaendelea. Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Afya wanatekeleza na kutoa elimu ya kinga, upimaji wa hiari na ushauri nasaha, matibabu kwa wanaoishi na VVU na kutoa huduma ya chakula kwa wagonjwa wa UKIMWI, huduma hii hutegemea uwepo wa bajeti. Pia kuna vikundi 15 vya wanaoishi na VVU na kati ya hivyo vikundi 5 ni vya watoto chini ya miaka 14 vilivyopo kituo cha AfyaTingi na Masoko pamoja na Hospital ya Wilaya na Shirika la dini.
Takwimu za maambukizi ya UKIMWI Kimkoa zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika Wilaya ya Kilwa kimepungua kutoka 2.8% mwaka 2007 hadi 2.1% kwa sasa (2016).
VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI
Kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2016Jumla ya akina mama 3,257 walijifungua. Kati ya hao 2,801 walijifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya.Vifo vya akina mama wajawazito na baada ya kujifungua ni 10.Vifo hivi vimesababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo, kina mama kuchelewa kufika katika vituo vya huduma, kifafa cha mimba na upungufu wa damu.
HALI YA UPATIKANAJI WA DAWA NA VIFAA TIBA
Jedwali linaloonyesha manunuzi ya dawa na vifaa tiba kwa miezi sita (Julai- Desemba 2016). Katika kipindi rejea cha taarifa jumla ya Tsh 290,337,835 zilitumika kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha kununulia dawa na vifaa tiba kwa vituo 53 vya kutolea huduma ya Afya. Pamoja na jitihada hizo bado kuna changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya dawa na vifaa tiba muhimu (Out of Stock) katika Bohari ya Madawa (MSD)
Chanzo cha pesa
|
Receipt in Kind (Ruzuku serikali kuu)
|
Fedha za Wafadhiri ( Basket Fund)
|
Fedha za uchangiaji (DRF, User fees)
|
CHF
|
Jumla
|
Kiasi cha pesa
|
98,156,255.88
|
159,014,900
|
21,163,980
|
12,002,700
|
290,337,835
|
Huduma za chanjo hutolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na akina mama wajawazito na wale walio katika umri wa kuzaa. Chanjo zinazotolewa vituoni ni aina saba ambazo zinakinga magonjwa yafuatayo, Kifua Kikuu, Pepopunda, Dondakoo, Kifaduro, Homa ya INI, Homa ya uti wa mgongo, Surua, Kichomi na kuhara kunakosababishwa na Rotavirus. Kwa Wilaya yetu, vituo 52 kati ya 55 vinatoa huduma ya chanjo. Kwa vituo visivyotoa huduma ya chanjo, wanapata huduma kwa njia za huduma mkoba (Out reach services).
Kwa kipindi cha Juni hadi Disemba 2016 kulikuwepo na chanjo za kutosha isipokuwa chanjo ya kukinga ugonjwa wa surua na kifua kikuu, kutokana upungufu wa chanjo hizo kwa ngazi ya Taifa na Mkoa. Walengwa wa chanjo ni kama ifuatavyo; Walengwa kwa mwaka ilikadiriwa kuwa watoto 8,002. Lengo kwa mwezi ni kuchanja watoto 667. Lengo la kitaifa ilikuwa kufikia zaidi ya 90% na Wilaya ya Kilwa imevuka lengo kwa chanja kwa asilimia 98.
Wilaya ya Kilwa inatekeleza agizo la Serikali, Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii ya Mwaka 2001 (CHF Act 2001) inayotaka kila mwanajamii kujiunga kwa hiari na mfuko wa Afya ya Jamii ambapo Wilaya imeanza kutekeleza mpango huu kuanzia mwaka 2006. Tangu mwaka huo viongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya hususani Idara ya Afya imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi juu ya faida ya kujiwekea bima ya Afya kabla ya kuugua.
Mfuko wa Afya ya Jamii unalenga kuwa na wanachama wa aina nne ambao ni:-
MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA (BRN)
Mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ni mkakati wa kitaifa wenye lengo la kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini vinakuwa na hadhi ya nyota walao 3 ifikapo Juni 2018. Katika Wilaya ya Kilwa vituo 55 viko katika mpango wa BRN kwa mgawanyiko ufuatao (Hospitali 2, vituo vya Afya 5 na Zahanati 48). Mikakati mbalimbali inafanyika ikiwemo, mafunzo kazini na vikao mbalimbali kwa watoa huduma za Afya juu ya umuhimu wa BRN pamoja na kutoa tafsiri ya viashiria vinavyotumika kupima ubora wa huduma zitolewazo vituoni. Aidha Simamizi Elekezi za Kitaifa, Mkoa na Kiwilaya zinaendelea kufanyika ili kuelekeza ni vigezo na viashiria gani hupelekea kituo kupata nyota kuanzia 1 na kuendelea.
MPANGO WA TATHIMINI SHIRIKISHI YA KIJAMII YA HUDUMA ZA AFYA (Community Scorecard).
Huu ni mpango wa Majaribio ufanywao kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) katika kuhakikisha wanajamii wanashirikishwa katika kutathimini ubora wa huduma za Afya ili kubaini changamoto zilizopo na kisha kuweka mikakati na mipango kazi ya kutatua changamoto hizo kwa kupitia jamii husika. Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa wilaya 6 za majiribio nchini katika Mikoa minne ya Lindi (Kilwa), Mtwara (Nanyumbu na Newala), Mbeya (Busokelo) na Tanga (Handeni na Bumbuli). Mradi huu unatekelezwa katika vijiji vya Mchakama, Kiwawa na Mandawa kwa wilaya ya Kilwa tangu mwaka 2016.
Lengo la mradi huu niKuongeza dhana ya ushirikishwaji na uwajibikaji kwa watoa huduma na wapokea huduma katika vituo vya huduma za Afya na kuondoa dhana ya kwamba kituo cha huduma za Afya ni mali ya Serikali.
Changamoto
Mikakati
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa