Wilaya ya Kilwa imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Usafishaji wa Mazingira Duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 20 Septemba, kwa kufanya shughuli mbalimbali za usafi katika maeneo ya stendi za mabasi na barabara kuu. Zoezi hilo limefanyika tarehe 20 Septemba 2025, likihusisha wananchi kutoka kata mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kufanya usafi wa pamoja.
Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo “TUNZA MAZINGIRA KWA KUZIPA TAKA THAMANI" ikilenga kuhamasisha jamii kutupa taka kwa usahihi na kuzuia uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha uchafuzi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Shija Lyela, amewapongeza Idara ya Mazingira na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni hiyo. Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na ni endelevu, hata katika siku za kawaida, ili kulinda afya za wananchi na kuboresha mandhari ya mji.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Boniface Achiula, amewashukuru wadau wote walioshiriki akisisitiza kuwa mshikamano wa jamii ni msingi muhimu katika kulinda mazingira. Pia ameahidi kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili kuhakikisha suala la usafi na uhifadhi wa mazingira linaendelea kuwa kipaumbele.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa