Watumishi wapya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa yamepatiwa mafunzo elekezi yenye lengo la kuwaongezea uelewa wa majukumu yao katika utumishi wa umma. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 22 Septemba 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Hemed Magaro amewataka watumishi hao wapya kutumia nafasi waliyoipata kwa bidii na uadilifu.
“Nawapongeza kwa kupata ajira hizi, ni nafasi ya heshima na dhamana kubwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ni wajibu wenu kuhakikisha mnafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya Utumishi wa Umma. Serikali inatarajia kuona matokeo chanya kupitia mchango wenu,” amesema Ndg. Magaro.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Wilaya ya Kilwa Ndg. Msena Bina amewasisitiza watumishi hao kuzingatia nidhamu na uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Washiriki yamepatiwa elimu kuhusu maadili ya utumishi wa umma, kanuni za kazi za serikali za mitaa, misingi ya maadili ya utendaji kazi, uwajibikaji, na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Aidha yamefundishwa mada maalum kuhusu makosa na adhabu katika utumishi wa umma, elimu ya afya ikiwemo Ukimwi mahala pa kazi, pamoja na masuala ya pensheni kwa watumishi wa umma.
Akitoa mafunzo hayo, mwezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi Mtwara Bwana. Gasper Kinsinza katika mada ya Makosa na Adhabu katika Utumishi wa Umma, amesisitiza umuhimu wa watumishi kufahamu taratibu na kanuni zinazowaongoza ili kuepuka makosa yanayoweza kusababisha hatua za kinidhamu.
Naye mwezeshaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF) Ndg. Yunus Buheti amewasihi washiriki kuzingatia mafunzo waliyoyapata na kuyatekeleza kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi wapya wanayatekeleza majukumu yao kwa weledi, kuzingatia sheria na taratibu, na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa