WILAYA YA KILWA YAPATA HATI SAFI 2017/2018
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoni Lindi imepata hati safi kutokana na ukaguzi iliyofanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG) katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2017/2018.
Akifungua Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashari ya Wilaya Kilwa Mhe.Abuu Mussa Mjaka aliwaelekeza wajumbe wa halmashauri kujikita kwenye hoja za CAG baada ya hoja hizo kujadiliwa katika kamati ya fedha na utawala.
Katika Baraza maalum la madiwani lililoitishwa kujadili hoja za ukaguzi za CAG ambalo pia limehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa Lindi Mhe.Godfrey Zambi ambapo Mkaguzi Mkuu mkazi kutoka ofisi ya CAG Ndg Musa Ally Musa aliwasilisha taarifa ya ukaguzi.
Akiwasilisha taarifa hiyo Ndg Musa Ally Musa alisema ofisi yake imeridhika na majibu ya hoja mbali mbali zilizowasilishwa huko nyumba ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iliwahi kupata hati chafu kutokana na hoja mbali mbali zilizowasilishwa.
Aliongeza kuwa , ofisi yake imeridhika na utekelezaji wa hoja mbali mbali zilizoibuliwa na hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imekidhi vigezo vya kupata hati safi na kuongeza kuwa ofisi yake inaagiza halmashauri kuendelea kutekeleza hoja ambazo bado zipo mezani.
Hoja zilizoibuliwa huko nyuma ni pamoja na ulipaji wa madeni ya mifuko ya kijamii kwa wafanyakazi, ulipaji wa asilimia kumi ya mikopo kwa ajili ya akina mama na vijana,ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja hoja ya uhaba wa watumishi katika idara mbali mbali za halmashauri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg Renatus Mchau ambaye ndiye msimamizi wa utekelezaji wa maagizo hayo alisema ofisi yake imejielekeza katika katika kuondoa hoja zote kulingana na aina ya hoja lakini pia kwa yale yaliyo nje ya uwezo wa ndani wa Halmashauri atajitahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi. sisi majukumu yetu makuu ni kuwahudumia wananchi hivyo tunajitahidi kuhakikisha huduma inayopatikana inafikia malengo yanayotarajiwa na serikali kuu pamoja na wananchi kwa ujumla aliongeza Ndg Mchau. Kuhusu uhaba wa watumishi, Mkurugenzi Mtendaji alisema ofisi yake inafanya mawasiliano na serikali na jitihada zimeshazaa matunda ambapo kuanzia mwaka jana jumla ya watumishi 205 wa fani mbali mbali wameajiriwa na wote wamesharipoti na kupangiwa majukum.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.Godfrey Zambi pamoja na pongezi aliwataka waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanashirikiana na timu ya menejimenti katika kusimamia mapato ya Halmashauri kwani vyanzo vyote vya Halmashauri vipo katika maeneo yao. Wahe.Madiwani ninyi ni viongozi, hakikisheni Halmashauri yenu inakusanya mapato ili kufikia malengo na mtakapofikia malengo kwa asilimia mia moja ni ninyi ndiyo mtapata sifa aliongeza Mhe.Zambi.
Naye katibu tawala wa mkoa wa Lindi Bi.Rehema Madenge alijikita katika kukemea mimba za utotoni kwani takwimu zinaonesha kuanzia Januari mwaka huu jumla ya watoto 28 wameripotiwa kupata ujauzito na kusikitishwa na taarifa za hivi karibuni za mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Nambondo kata ya Mingumbi kupata ujauzito. Bi Rehema aliwaasa waheshimiwa madiwani kuhakikisha hawa watu wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Vyanzo vikuu vya mapato vya Halmashauri ya Wilaya Kilwa Kilimo cha ufuta, korosho ,uvuvi katika bahari ya Hindi pamoja mapato yanayotokana na mazao ya misitu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa