Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, ameonyesha kufurahishwa na maandalizi na ubora wa viwanja vya maonesho ya Nane nane Kanda ya Kusini, vilivyopo Ngongo, Mkoani Lindi.
Akizungumza wakati wa kilele cha maonesho hayo yaliyofanyika tarehe 8 Agosti 2025, Mhe. Jafo ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesifu kwa dhati juhudi za mikoa ya Lindi na Mtwara katika kuhakikisha viwanja hivyo vinakuwa vya kisasa, vyenye miundombinu bora ikiwemo barabara za lami, hali inayochochea ubora wa viwanja hivyo.
“Mmeweka alama ya kipekee kwa kuandaa viwanja vyenye hadhi na vigezo bora kwa maonesho haya. Hii ni hatua muhimu katika kutangaza fursa na kuhamasisha uendelezaji wa sekta ya kilimo na uchumi wa viwanda,” amesema Mhe. Jafo.
Katika hotuba yake, Mhe Jafo pia amezipongeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa mikopo hiyo imekuwa kichocheo kikubwa katika kuimarisha biashara ndogondogo, shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Akizungumzia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Jafo ameeleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 626 zimetolewa kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za kilimo, ambapo zaidi ya asilimia 85 ya pembejeo hizo zimeelekezwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, hususan kwa mazao ya kimkakati kama korosho.
Aidha, amewataka wananchi wa Kanda ya Kusini kutumia maarifa na teknolojia walizojifunza kupitia maonesho haya ya nane nane ili kuongeza tija katika uzalishaji, kuongeza kipato na kuchangia ustawi wa jamii.
Maonesho ya Nane nane kwa mwaka 2025 yameendeshwa kwa kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa