Ofisi ya Utumishi na Utawala bora kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imeendesha mafunzo ya siku moja kwa watumishi wa umma juu ya matumizi ya Mfumo wa Pepmis (Performance Management Information System), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa utendaji kazi serikalini.
Mafunzo hayo yamefanyika Tarehe 13 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mkapa uliopo katika Shule ya Sekondari Masoko, yakihusisha watumishi kutoka idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha watumishi kuelewa kwa kina namna ya kutumia mfumo huo katika kupanga, kutekeleza na kutathmini utendaji kazi wao kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwezeshaji kutoka Wizara ya Utumishi Ndg.Mutani Manyama ameeleza kuwa mfumo wa PEPMIS ni sehemu ya mageuzi ya kiutendaji yanayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa umma.
“Mfumo huu utarahisisha ufuatiliaji wa malengo ya kila mtumishi na kutoa nafasi kwa viongozi wa idara kufanya tathmini kwa wakati, jambo ambalo litaongeza ufanisi na uwajibikaji kazini,” amesema. Ndg. Manyama
Watumishi walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira ya kuwajengea uwezo wa kiteknolojia, wakisema mfumo huo utawasaidia kurahisisha kazi na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi kwa wakati.
Mafunzo kama haya yanatarajiwa kuendelea kutolewa katika maeneo mengine nchini ili kuhakikisha kuwa watumishi wote wa umma wanakuwa na ujuzi sahihi wa kutumia mifumo ya kidijitali katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa