Kilwa
Watumishi wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya utendaji na kitaaluma katika utumishi wa umma.
Wito huo umetolewa na Afisa utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Ally Ligalawike alipokua akizungumza na Watumishi katika Semina elekezi ya Mafunzo kwa Watumishi wapya iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Kinyonga Mjini Kilwa Kivinje.
Ligalawike amesema iwapo watafuata misingi na kanuni zilizowekwa katika utumishi wa umma basi watafanya kazi bila shaka na wasiwasi wowote.
”Katika utuimishi wa umma kuna kanuni na Sheria ambazo zinatuongoza kama walivyoelezea wawezeshaji waliopita kwahiyo kama utakua unazikiuka hizo kanuni na maadili basi moja kwa moja utaadhibiwa kutokana na sheria inavyosema na sidhani kama utaweza kuwa huru au kujisikia vizuri kama utakua unapewa Onyo mara kwa mara juu ya mienendo yako katika utumishi lazima utakua mtu wa wasiwasi” alisema Ligalawike
Pia amewataka watumishi hao kuwa na heshima na nidhamu kwa watu wote na kuwahudumia bila kujali itikadi zao
”Wengi wetu hapa ni vijana na kama mnavyojua vijana kuna maneno Fulani ambayo tunapenda kuyatumia, sitarajii kusikia tunatumia maneno ya mtaani sehemu ya kazi Mfano anakuja mgonjwa unaanza kukamkaribisha kwa salamu za vijiweni oi niaje? Au kaja mtu kavalia suti nzuri kama rafiki yangu hapo ukaona yes! huyu ndiye wa kuanza kumpa huduma ukawaacha wengine ambao amewakuta katika utaratibu mambo hayo hakuna” alisisitiza Ligalawike
Afisa utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Ally Ligalawike akizungumza na Watumishi kutoka Idara ya Afya katika Semina elekezi ya Mafunzo kwa Watumishi wapya iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Kinyonga Mjini Kilwa Kivinje (Picha: Ally Ruambo)
Aidha amewataka kuzingatia Mavazi ambayo Mtumishi wa umma ameruhusiwa kuvaa na kuheshimu pamoja na kutunza mali na siri za ofisi.
“Kuna taarifa ambazo zinatakiwa kuwa wazi ili wananchi wazijue kama vile mapato na matumizi ya vituo vyetu vya kutolea Huduma na kuna Taarifa zingine zinabaki kuwa siri ya ofisi, ni kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa Umma kuvujisha siri za ofisi kwahiyo naomba muwe makini sana na suala hili” alihitimisha ligalawike .
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi waliohudhuria mafunzo hayo Muhasibu msaidizi kituo cha afya Masoko Nuru Mwamakula amesema wanashukuru kwa mafunzo waliyoyapata kwani yamewaongezea uwezo zaidi katika utekelezaji wao wa majukumu yao ya kila siku.
“Mimi binafsi na wenzangu tunashukuru kwa mafunzo kwani haya mafunzo yametutoa sehemu moja na kutupeleka sehemu nyingine ambayo ni bora zaidi, kuna mambo ambayo yalikua yanafanyika labda kwa kuto kujua lakini kwa sasa naimani hayataweza kujitokeza tena
Mimi binafsi muda mrefu sana nimekua nikifanya kazi katika taasisi binafsi kwahiyo kuna mambo ambayo nilitoka nayo na kuja nayo huku bila kujua kuwa utaratibu ni tofauti kidogo kwa kua nilikua sifahamu lakini kwa mafunzo haya sasa nimekua mpya” alisema Nuru
Muhasibu msaidizi kituo cha afya Masoko Bw. Nuru Mwamakula akizungumza katika Semina elekezi ya Mafunzo kwa Watumishi wapya iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Kinyonga Mjini Kilwa Kivinje (Picha: Ally Ruambo)
Awali akizungumza na watumishi Katibu wa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Maongezi amewataka watumishi kuwa wawazi pindi wapatapo changamoto katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kufuata ngazi katika kuwasilisha matatizo yao.
“Hili ni jambo muhimu sana ndugu zangu msikae na matatizo sisi viongozi tupo tuelezeni na tutawasaidia ila tu niwakumbushe kufuata utaratibu. Kuna wengine wakiwa na jambo lao moja kwa moja wanaenda ngazi za juu mwisho wa siku shauri linarudishwa chinimkwa kua sisi ndio wa kwanza kuyajibia, kwahiyo tufuate utaratibu” alisema Maongezi
Pia amewapongeza watumishi hao wa utendaji wao wa kazi kwani kwa muda mfupi ambao wameajiriwa matokeo Chanya yameanza kuonekana katika vituo vyao vya kazi.
“Kwa hili niwapongeze kwa muda mfupi ambao tumekuwa pamoja katika utendaji tumeona mabadiliko kwahiyo naomba muendelee na spidi hiyo hiyo na ikiwezekana muzidishe zaidi” alisema Maongezi
Katibu wa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Maongezi akizungumza na Watumishi kutoka Idara ya Afya katika Semina elekezi ya Mafunzo kwa Watumishi wapya iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Kinyonga Mjini Kilwa Kivinje (Picha: Ally Ruambo)
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya wilaya ya Kilwa Bi. Zabib Uledi amewataka watumishi hao kutoshiriki katika vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya, Pombe kupindukia, uasharati pamoja na vitendo vya rushwa.
Katibu wa Hospitali ya wilaya ya Kilwa Bi. Zabib akitoa maelekezo kwa Watumishi katika Semina elekezi ya Mafunzo kwa Watumishi wapya iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Kinyonga Mjini Kilwa Kivinje (Picha: Ally Ruambo)
Zaidi ya Watumishi kumi na tano kutoka vituombalimbali vya Afya wakiwemo Wahasibu , Wataalamu wa Maabara na Wauguzi wamepatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo Haki na wajibu wa Mtumishi,Majukumu, Kanuni za Maadili ya utendaji na kitaaluma katika utumishi wa umma, nidhamu, usiri, utunzaji nyaraka, mavazi, na mengine mengi.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa