Jopo la Wataalamu wa Elimu kutoka Wilaya ya Rufiji wamefanya ziara maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu za kuboresha viwango vya ufahulu kwa wanafunzi wa Elimu ya Sekondari katika maeneo yao. Ziara hiyo imewakutanisha Maafisa Elimu ngazi ya Wilaya na Kata, Walimu Wakuu na Walimu wa Taaluma wa Shule za Sekondari kutoka Wilaya ya Kilwa na Rufiji ambapo wamejadili Mikakati iliyosaidia kuongeza ufaulu katika Shule za Sekondari wilayani Kilwa. Ziara hiyo imefanyika leo Tarehe 13/03/2025 katika Shule ya Sekondari Kilwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Elimu Taaluma Wilaya ya Kilwa Ndg. Flavian Bujiku ameeleza kuwa, moja ya siri ya mafanikio yao katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Shule za Sekondari Wilayani Kilwa ni ushirikiano mzuri kati ya Viongozi wa Halmashauri na Walimu, jambo ambalo limeleta Motisha na kuongeza uwajibikaji katika kazi. Pia Ndg. Bujiku amesema kuwa hatua Madhubuti walizozichukua katika kuhakikisha wanafuta daraja sifuri katika shule nyingi wilayani Kilwa ni Uanzishaji wa kambi za masomo mashuleni ambazo zimesaidia kuongeza muda wa kujifunza na kufanya mazoezi ya Mitihani kwa muda mwingi.
Kwa upande wao Walimu Wakuu na walimu wa taaluma Wilaya ya Kilwa wamesema mbinu nyingine wanazozitumia ni pamoja na kuwaelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni, hatua inayochangia kuboresha afya na umakini wa wanafunzi darasani. Pia Waalimu hao wamesema mbali na mbinu hizo pia walimu wanajitoa kwa dhati kuhakikisha wanafunzi wanaelewa masomo yao.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Rufiji Bi. Theresia Charles amewashukuru Walimu na Maafisa Elimu wa Wilaya ya Kilwa kwa kuwapa mbinu madhubuti za kuinua ufaulu kwa wanafunzi na kuwataka waalimu wa Wilaya ya Rufiji kutumia maarifa na mbinu walizozipata kutoka kwa waalimu wenzao ili kuboresha ufaulu katika Wilaya yao.
Kwasasa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha inatokomeza daraja sifuri katika shule za sekondari kama vile Shule ya Sekondari Kivinje, Shule ya Sekondari Miguruwe, Shule ya Sekondari Ilulu na Shule ya Sekondari ya Kiislam Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa