Katika kuhitimisha mafunzo ya siku mbili kwa waongoza watalii wilayani Kilwa, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtei, ametoa wito kwa wadau wa utalii kutumia kikamilifu elimu waliyoipata ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya utalii ndani ya wilaya hiyo na nchini kwa ujumla.
Amezungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo tarehe 23/05/2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa, Dkt. Florin Mtei amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati ya muda mrefu kuhusu maendeleo ya utalii kutokana na Serikali kuandaa miradi mikubwa itakayoenda kukuza shughuli za utalii ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege na bandari ya kisasa ya uvuvi, ambayo ni fursa adhimu kwa Wilaya ya Kilwa katika kujiimarisha kama moja ya vivutio vya kipekee kwa watalii wa ndani na kimataifa.
"Kilwa ni eneo lenye historia na rasilimali za kipekee. Mafunzo haya ni hatua ya msingi katika kuwajengea uwezo waongoza watalii ili wawe mabalozi wa utalii wetu. Tunatarajia kuona mabadiliko ya kweli kupitia ubunifu, ukarimu na umahiri wa kuwasiliana na wageni," amesema Dkt. Florian.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Kilwa Ndg. Yusuf Mwinyi akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa serikali imejipanga kuboresha zaidi mazingira ya sekta ya utalii, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, kuimarisha huduma za kijamii, pamoja na kushirikisha jamii kikamilifu katika shughuli za kitalii ili kunufaika kiuchumi na kijamii.
Afisa Utalii wa Wilaya ya Kilwa Ndg. Phabian Boniphace ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa ya manufaa makubwa kwa washiriki, kwani yameongeza maarifa kuhusu namna ya kutoa huduma bora kwa wageni, kukuza ubunifu katika bidhaa za utalii, pamoja na kuboresha uelewa wa lugha za kigeni kutokana na mafunzo hayo ya siku mbili.
Mmoja wa waongoza watalii waliopatiwa mafunzo Ndg. Samweli Moja amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa kwa kina namna ya kuhudumia wageni kwa viwango vya kimataifa,ukarimu na kujifunza umuhimu wa kuitangaza Kilwa kwa kuihusisha jamii kushiriki katika shughuli hizo za kitalii.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa