Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika kila mwaka Tarehe 08 mwezi Machi, Wanawake Kata ya Masoko Wilayani Kilwa wametakiwa kugawanya majukumu yao ya Kiuchumi na Kifamilia kwa usawa ili kusaidia utunzaji wa familia zao ikiwemo kutimizia mahitaji ya watoto kama kuhakikisha wanapata elimu, chakula na kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia unaotokea katika jamii,
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg. Stella Omari Leo tarehe 03/03/2025 Katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Kata yaliyobeba Kauli mbiu inayosema ‘‘WANAWAKE NA WASICHANA 2025 TUIMARISHE HAKI, USAWA NA UWEZESHAJI’’. Maadhimisho hayo yamefanyika katika kata ya Masoko, Mtaa wa Mihina, ambapo yamehusisha shughuli mbalimbali ikiwemo Usafi katika eneo la ujenzi wa Shule ya Msingi Mihina, Utoaji wa Elimu na Vifaa vya kusomea kwa watoto wa kike walio na Uhitaji Maalumu katika kata ya masoko.
Pia Ndg. Stella ametoa wito kwa wanawake hao kuachana na tamaduni zinazo mkandamiza mwanamke pia kujitokeza katika nafasi mbalimbali ikiwemo kugombea nafasi za uongozi kwani hiyo ni haki yao ya msingi na itasaidia kuleta usawa unaotakiwa kuwepo kati ya mwanamke na mwanaume katika jamii.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Ndg. Paul Hilary amewataka wanawake kata ya Masoko kutumia Nishati safi na salama ya kupikia ili kulinda Afya zao na kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya nishati isiyo salama ikiwemo ukataji wa miti kwaajili ya kuni na mkaa katika misitu.
Aidha Ndg. Zulfa Makame kwa niaba ya Afisa Mtendaji kata ametoa pongezi kwa wanawake wa Kata ya Masoko kwa muamko walioonyesha katika kushiriki zoezi la usafi eneo la ujenzi wa shule msingi Mihina, Pia amewaomba kuendelea kujitoa na kushirikiana katika shughuli nyingine za kimaendeleo kwaajili ya maendeleo ya kata hiyo na Taifa kwa ujumla.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa