Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Hemed S. Magaro, amekabidhi pikipiki tano (5)kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wilayani Kilwa kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 09 Septemba 2025 katika ukumbi wa TUJIWAKI mara baada ya kikao cha Maafisa Maendeleo ya Jamii kilicholenga kujadili na kukumbushana majukumu ya idara hiyo, ikiwemo suala la uwajibikaji na usimamizi wa shughuli za utoaji mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali wilayani Kilwa.
Kikao hicho pia kimelenga kuweka mikakati ya namna ya kuboresha upatikanaji wa huduma kwa jamii, ambapo pikipiki hizo zinatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza kasi ya Maafisa kufika vijijini, kufuatilia shughuli za maendeleo, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Baada ya makabidhiano hayo Ndg. Magaro amewataka Maafisa hao kuhakikisha wanazitumia pikipiki hizo kwa matumizi sahihi na kwa uangalifu mkubwa, ili ziweze kudumu na kusaidia katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.
Aidha, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, siyo tu kwenye usimamizi wa mikopo ya vikundi, bali pia katika kutekeleza shughuli zote za kijamii zinazolenga kuinua ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Kilwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Grace Mwambe ameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi kwa kuwaongezea vitendea kazi na kuahidi kuwa idara hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa bidii, weledi na uwajibikaji mkubwa kwa manufaa ya wananchi wa Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa