Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, Afisa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Ndugu Jihadhari Said Mwinishehe, amekutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa wa Wilaya ya Kilwa kwa ajili ya kikao cha elimu na maelekezo muhimu ya kuelekea uchaguzi.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) – Kilwa, tarehe 02 Septemba 2025.
Lengo kuu la kikao hicho ni kuwakumbusha Viongozi wa Vyama vya Siasa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi, kuhimiza kampeni za amani na kuepuka vitendo vya uchochezi au matumizi ya lugha za chuki.
Aidha, kikao kimeweka msisitizo wa kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu taratibu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa rai kwa vyama vyote kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi na uwajibikaji, huku viongozi wa vyama wakihimizwa kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha mshikamano wa kitaifa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa