Katika kuendeleza vipaji vya michezo kwa wasichana wilayani Kilwa, timu ya wasichana "Kilwa Princess" imezinduliwa rasmi na kufanya harambee maalum ya kuchangisha fedha na vifaa ili kuiwezesha timu hiyo kufikia mafanikio ya juu katika tasnia ya michezo.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Mashujaa Business Centre, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Ndg. Yusuf Mwinyi, aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ndg, Juma Muhando ameeleza mafanikio ya awali ya timu hiyo huku akiiomba serikali na wadau wa michezo kuisaidia timu kwa mahitaji muhimu ikiwemo vifaa vya kufanyia mazoezi kwa vile jezi za michezo, mipira, pamoja na bajeti kwa ajili ya safari za kimichezo ili kuiwezesha kushiriki mashindano mbalimbali kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Ndg. Yusuf Mwinyi, amesema kuwa serikali iko tayari kuiunga mkono timu hiyo , ikiwa ni sehemu ya juhudi katika kuinua michezo kwa wasichana na vijana kwa ujumla. Pia ametoa wito kwa wadau wa michezo, mashirika binafsi, taasisi za kijamii, na watu binafsi kujitokeza kwa wingi ili kusaidia timu hiyo chipukizi.
Naye Afisa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Wilaya ya Kilwa, Bi. Veneranda Maro, ameipongeza timu ya Kilwa Princess kwa uthubutu wao wa kujitokeza na kuanzisha timu hiyo ya wasichana, hatua aliyosema ni muhimu kwa maendeleo ya michezo ya wanawake nchini. Amewahimiza wachezaji kuzingatia nidhamu, bidii, na kujituma zaidi ili kufikia viwango vya juu vya kitaifa na kimataifa.
Katika harambee hiyo, michango mbalimbali ilitolewa, ikiwemo fedha taslimu na vifaa vya michezo, huku baadhi ya wadau wakiahidi kuendelea kutoa msaada wa mara kwa mara kwa timu hiyo.
Kilwa Princess ni moja ya timu ya wasichana wilayani Kilwa ambayo imeanzishwa kwa lengo la kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo miongoni mwa wasichana, pamoja na kuwapa nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya kijamii kupitia michezo hiyo
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa