Wakulima wa zao la ufuta Wilayani Kilwa wameipongeza Halmashauri ya Wilaya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kwa kuanzisha mfumo mpya wa Mnada katika ununuzi wa zao hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Wakulima, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Kibaoni Amcos Bw. Adam Chumi amesema wamefurahishwa sana na uamuzi wa Halmashauri na Mkoa wa kuanzisha mfumo wa Mnada.
Adam amesema mifumo ambayo ilikua inatumika katika ununuzi Ufuta ilikuwa inawakandamiza sana na haikuwa na tija kwao hali ambayo ilikuwa inawakatisha tamaa ya kuendelea na kilimo cha ufuta.
”Tunaishukuru sana Halmashauri yetu kwa kuunga Mkono wazo la kutumia Mfumo wa mnada katika uuzaji wa ufuta kwa sababu lina tija kwetu sisi kama wakulima.
Kwa miaka yote ambayo tumekuwa tunalima ufuta hatujawahi kuuza kilo ikazidi Shilingi 2000 lakini kama mlivyoona pale kwenye Mnada kuwa Ufuta utanunuliwa kwa Shilingi 2815 kwa Kilo jambo ambalo tulikuwa tunaliota miaka mingi.
Mwaka jana mimi na wenzangu wachache tuligoma kuuza Ufuta wetu kwa Shilingi 1650 kwa Kilo, tulikaa nao sana mwishoni tukauza kwa Shilingi 1850 kwa Kilo sasa unaweza kuona mwenyewe mabadiliko yaliyoletwa na huu mfumo”. Alisema Adam
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Bw. Charles Kabeho akifungua Bahasha za Barua za maombi kujua kampuni iliyoshinda kununua Ufuta Wilayani Kilwa. (Picha :Ally Ruambo)
Aidha Adam ameupongeza mfumo jinsi unavyo fanya malipo ambapo mkulima anaingiziwa pesa katika akaunti yake baada ya mnada.
“Awali Mfanyabiashara alikua anakulipa fedha tasilimu mkononi jambo ambalo kwa usalama halikuwa zuri lakini pia wengi wao walikua wanakuja na Mizani ambazo zimechezewa swala ambalo lilikua linaongeza unyonyaji kwa mkulima” aliongeza Adam
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 Bw. Charles Kabeho (Kushoto) akizungumza na Wananchi wakati wa uzinduizi wa Mradi wa uuzaji wa zao la Ufuta kwa njia ya Mnada Wilayani Kilwa, Kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai (Picha:Ally Ruambo)
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Zablon Bugingo amewataka Wakulima kutumia fedha zao kwa nidhamu ili ziweze kuwasaidia kuboresha maisha yao na kuwakumbusha kuweka akiba kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao
“Fedha ambazo mtazipata msizifuje, zitumieni kwa nidhamu ya hali ya juu na mkumbuke kuwa kuna msimu mwingine ambao nao unahitaji maandalizi ya mapema, Sitarajii kusikia kuna mkulima ametumia pesa zote akakosa hata pesa ya akiba ambayo itamuwezesha kugharamia gharama za kuanzisha tena kilimo msimu ujao” alisema Bugingo.
Mnada wa uuzaji wa Ufuta katika kijiji cha Zinga Kibaoni wilayani Kilwa ni miongoni mwa Miradi iliyozinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa