Afisa Mwandikishaji Wilaya ya Kilwa, Ndg.Msena Bina, Tarehe 14 Mei 2025 amewaapisha Waandishi wasaidizi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Awamu ya pili ambapo zoezi hilo limefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Ndg. Bina amewataka waandishi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza siri za kazi pamoja na vifaa vya kazi watakavyotumia wakati wa zoezi hilo muhimu la kitaifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg Hemed Magaro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika uandikishaji,huku akitoa maagizo kwa waandishi ngazi ya kata kuhakikisha wanatumia makundi manne ambayo ni shule, viongozi wa dini, Wenyeviti wa Vitongoji na Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kuweza kusaidia taarifa hiyo kufika kwa haraka wananchi.
“Ni muhimu taarifa kuhusu uandikishaji ziwafikie wananchi wote kwa haraka na kwa ufanisi. zoezi hili ni la kitaifa na kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu” amesema Ndg. Magaro
Aidha, baada ya zoezi la kuapishwa, waandishi wasaidizi hao wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya uandikishaji, ikiwemo namna ya kutumia Mfumo wa Usajili wa Wapiga Kura (VRS) ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.
Zoezi hilo litafanyika kwa siku 7 kuanzia tarehe 16 Mei 2025 hadi tarehe 22 Mei 2025 Vituo vya kuandikishia wapiga kura vimepangwa katika kila Kata na vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa