Mkuu wa mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi amewataka wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyomiliki Misitu kuweka mipango endelevu ya kuhifadhi Misitu hiyo.
Wito huo ameutoa leo Novemba Mosi, katika Hafla fupi ya kukabidhi Mtambo wa kukaushia Mbao wenye thamani ya Milioni Mia Moja Ishirini kwa Vijiji Kumi na moja vinavyomiliki misitu, Hafla iliyofanyika katika viunga vya Halmashauri ya wilaya ya Kilwa.
Zambi amewataka wanavijiji hao kuhifadhi misitu hiyo kwa manufaa ya kizazi kilichopo sasa na kizazi kitakacho kuja.
“Msije mkaingiwa na tamaa mkafyeka Misitu yote kwa ajili ya kuuza mbao na matumizi mengine mpaka vizazi vijavyo vikaja kusikia historia tu kuwa hapa zamani kulikuwa na msitu mkubwa” alisema Zambi
Pia Mhe. Zambi amewataka Viongozi ambao wanaongoza vijiji ambavyo vinamiliki Misitu kuwa waaminifu kwa wanainchi wanao waongoza kwa kutumia vizuri dhamana waliyopewa kwa kufanya kazi kwa bidii , uaminifu na uwazi
Zambi amesema kuna baadhi ya viongozi wa Vijiji ambao sio waaminifu wamekuwa wakivuna Miti na kuuza mbao kwa maslahi yao binafsi kitu ambacho ni kinyume na maadili na kuahidi kwa chukulia hatua za kisheria wote watakao bainika kufanya vitendo hivyo.
“Kuna baadhi ya vijiji tumewakamata na kuwaweka ndani viongozi wao, wanavuna mboa na kuziuza kwa maslahi yao binafsi na Kijiji hakifaidiki na chochote. Serikali haiwezi kuvifumbia macho vitendo hivi, tutawakamata na kuwafikisha sehemu husika” alisisitiza Zambi
Aidha Zambi amevitaka vijiji hivyo kuvuna Miti ambayo imekomaa kwa ajili ya matumizi na kuwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanakabiliana na wavamizi wanao vuna misitu kinyume na Utaratibu.
“Angalieni mfano mzuri kijiji cha Nanjirinji wametunza misitu na wamefaidika, wamejenga Ofisi ya kijiji wameanzisha mradi wa nyumba ya kulala wageni, wana wasaidia wanafunzi ambao wanafaulu kuendelea na masomo lakini pia wana wasaidia wamama wajawazito igeni mfano huu” alihitimisha Zambi
Mkuu wa mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi akiwasha Mtambo wa kukaushia Mbao kuashiria kuanza kutumika rasmi kwa Mtambo huo katika Hafla fupi iliyofanyika katika viunga vya Halmashauri ya wilaya ya Kilwa (Picha na: Ally Ruambo)
Awali akizungumza katika Hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai amevitaka Vijiji kuendelea kutunza Misitu kwa kupanda Miti mingine baada ya kuvuna na kuzielekeza pesa katika shughuli za kimaendeleo baada ya mauzo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya kilwa Bw. Hatibu Ramadhani ameishukuru taasisi ya Mipingo kwa juhudi wanazofanya katika kuhifadhi misitu na misaada wanayoendelea kuipatia Halmashauri ya wilaya ya kilwa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa