Umasikini Siyo Sifa , Tusibweteke –Ngubiagai
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe.Christopher Ngubiagai , ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa kutobweteka na miradi inayosimamiwa na mpango wa kunufaisha kaya masikini Tanzania-TASAF kwani mpango huo ni kwa kaya masikini tu.
Mhe.Ngubiagai ameyasema hayo katika ufunguzi wa semina ya siku moja kwa Waheshimiwa madiwani ,waratibuwa TASAF pamoja na wakuu wa idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Katika semina hiyo, Mhe.Ngubiagai aliwataadharisha pia waratibu watakaohusika katika zoezi la utambuzi wa kaya masikini kutenda haki ili watakaopatikana wawe kweli ni walengwa badala ya kuingiza watu wasiokuwa na sifa. ‘’Ndugu zangu mmeaminiwa , naombeni mkatende haki huko muendako, msionee wala kumpendelea mtu’’ aliongeza Mhe.Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF Bi. Janeth Madulu, amesema katika awamu hii ya pili ya TASAF awamu ya tatu vijiji vyote tisini katika Wilaya ya Kilwa vitafikiwa na wahitaji wote wataingizwa katika mpango. Mwakilishi huyo aliwaeleza washiriki kuwa ,katika mipango ya awali ya TASAF imepata manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha umasikini Tanzania bara na Visiwani kwa asilimia sabini jambo ambalo ni hatua kubwa katika utekelezaji.
‘’Kila mwaka tumekuwa tukiwandoa baadhi ya kaya katika orodha ya wanufaika katika mpango wa TASAF , hii ni kutokana na kuhitimu katika hatua za awali’’ , Bi. Janeth Madulu aliongeza kuwa hawa wahitimu ni wale ambao wamefanikiwa kuondoka katika viwango vya chini vya umasikini.
Aliongeza kuwa awamu hii inalenga kufikia kaya milioni moja, laki nne na elfu hamsini ambapo Zaidi ya wanufaika milioni saba wanatarajiwa kufikiwa nchi nzima , hii ni katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara pamoja na Pemba na Unguja.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ambaye pia ni diwani wa kata ya Miguruwe Mhe.Farida Kikoleka amewashauri wasimamizi wa TASAF katika ngazi ya Wilaya kuzingatia upatikanaji wa mitandao ya simu kwani mpaka sasa Zaidi ya vijiji kumi katika Wilaya ya Kilwa havina mawasiliano ya aina yoyote ya simu na hivyo inawawia vigumu kuwafikia wanufaika kwa njia ya simu.
‘’Nakubaliana na mpango wenu wa kuwahudumia wanufaika kwa njia ya mitandao kwa kuwatumia hela kwenye simu zao , lakini Wilaya yetu bado ina changamoto ya mawasiliano, hivyo tafuteni njia mbadala ya kuwafikia wanufaika wanaoishi katika maeneo haya ili kupunguza malalamiko ya wananchi’’ aliongeza Mhe.Kikoleka .
Mratibu wa TASAF katika halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bi. Mwanaidi Salu amesema mpaka sasa Zaidi ya kaya elfu nne zinahudumiwa katika Halmashauri ya Wilaya Kilwa ambapo Zaidi ya shilingi milioni mia sita(600,000,000) zinatolewa kwa wanufaika kwa kila mwaka.
Wilaya ya Kilwa ina jumla ya tarafa sita, kata ishirini na tatu, vijiji tisini na vitongoji 351.
Katika awamu ya kwanza wa utekelezaji wa mpango wa kupunguza umasikini nchini Tanzania –TASAF vijiji vilivyofikiwa katika Wilaya ya Kilwa ni 52 kati ya vijiji ambapo vijiji 38 havikuwa kwenye mpango wa awali kutokana na sababu mbali mbali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa