Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kupitia Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira imeendelea kutoa mafunzo ya kitaalamu kuhusu ufugaji nyuki, sambamba na kufanya ukaguzi wa mizinga katika misitu ya mikoko iliyoko katika maeneo ya ukanda wa pwani. Zoezi hili ni sehemu ya mkakati mpana unaolenga kukuza uchumi wa wananchi kupitia shughuli za ufugaji nyuki huku mazingira ya baharini na misitu ya mikoko yakihifadhiwa kwa njia endelevu.
Mafunzo haya yanawajengea uwezo wananchi kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira, pamoja na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa nyuki katika utunzaji wa mfumo wa ikolojia, hasa katika maeneo ya mikoko ambayo ni mazalia muhimu ya samaki na viumbe hai wa baharini.
Kwa mujibu wa maafisa kutoka Kitengo cha Maliasili, zoezi la ukaguzi wa mizinga lina lengo la kuhakikisha kuwa vifaa vya kufugia nyuki vinaendana na viwango vya kitaalamu na havileti madhara kwa mazingira. Aidha, hatua hii inalenga kuimarisha uzalishaji wa asali na bidhaa nyingine zitokanazo na nyuki, hivyo kuwa chanzo cha kipato kwa kaya za vijijini.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imekuwa mstari wa mbele katika kusisitiza ushirikiano baina ya jamii na taasisi za serikali katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira. Kwa mantiki hiyo, Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira kinatoa wito kwa wadau wote ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na wananchi – kushiriki kikamilifu katika kuendeleza elimu ya ufugaji nyuki kwa lengo la kuifikisha kwa jamii pana zaidi.
Mradi huu unatarajiwa kuchangia katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu hususan Malengo ya kutokomeza Umaskini,13 Kuchukua Hatua Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi.
Juhudi hizi ni ushahidi wa dhamira ya Halmashauri ya Kilwa katika kuunganisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na ajenda ya utunzaji wa mazingira, kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa