TANZIA
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha aliyewahi kuwa Diwani wa kata ya Nanjilinji na Mwenyekiti wa Halmashuri ya wilaya ya Kilwa Ndg. Ally Mtopa
Mzee Ally Mtopa amefikwa na umauti siku ya jumatatu tarehe 09.04.2018 katika hosptali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mzee Ally Mtopa aliwahi kuhudumu katika nafasi ya Udiwani wa kata ya Nanjilinji, wilayani kilwa kutoka mwaka 1995 hadi 2015 na wakati huo huo kwa umahiri wake katika ungozi alipewa dhamana ya Uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Pia mzee Ally Mtopa aliwahi kuhudumu katika chama cha mapinduzi (CCM) tangu zama za TANU ambapo alikua Mwenyekiti wa TANU Wilaya ya Kilwa mwaka 1974 hadi mwaka 1977. Baada ya kushiriki kuasisi CCM alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilwa kwa kipindi cha miaka 20 kutoka mwaka 19977 hadi mwaka 1997.
Vilevile mzee Mtopa alihudumu kama Mwenyekiti wa wa CCM Mkoa wa Lindi kwa miaka 14 tangu mwaka 2003 ambapo pia kwa utaratibu wa kipindi hicho alikua Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM kati ya mwaka 2007 na 2012.
Sanjari na kushiriki harakati za kupigania uhuru wa taifa letu na kuasisi chama cha mapinduzi (CCM) mzee Mtopa amedumu kama mshauri wa chama na viongozi wa chama ngazi za msingi mpaka taifa.
Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa chini ya mkuu wa Wilaya Mhe. Christopher Ngubiagai, Mweneyekiti wa halmashauri Mhe. Abuu musa Mjaka na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya kilwa Ndg. Zablon Bugingo unatoa salamu za pole kwa familia ya marehemu , ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huu, Mungu awape ustahamilivu na nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema.
Amin.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa