Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia Mei 1 hadi Julai 4, 2025, ili kutoa fursa kwa wananchi kujiandikisha, kurekebisha taarifa na kutoa pingamizi dhidi ya wasio na sifa.
Akizungumza leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Mhe. Jacobs Mwambegele amesema zoezi hilo litafanyika kwa mizunguko mitatu, ambapo mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15, wa pili mikoa 16, na wa tatu vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo Tanzania Bara na Zanzibar.
Mhe. Jaji Mwambegele amebainisha kuwa jumla ya vituo 7,869 vitatumika katika zoezi hili, ambapo vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Zanzibar. Tume inatarajia kuwaandikisha wapiga kura wapya 1,396,609, huku wapiga kura 1,092,383 wakiboresha taarifa zao na 148,624 wakiondolewa kwa kukosa sifa.
Uboreshaji huo utafanyika katika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Zanzibar, na utahusisha pia utoaji wa kadi mpya kwa waliopoteza au kuharibu, pamoja na kuwapa nafasi wapiga kura kuhama maeneo yao ya awali au kufanya marekebisho ya taarifa binafsi.
Aidha, Daftari la Awali la Wapiga Kura litawekwa wazi kwa umma kupitia vituo vyote vilivyotumika katika awamu ya kwanza ya uboreshaji, ili kuruhusu ukaguzi, marekebisho na pingamizi kwa waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa, kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inawahamasisha wananchi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa haki yao ya kidemokrasia, kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa