Taasisi ya Tanzania Agroforestry and Marine Conservation Organization (TAMCO) kwa kushirikiana na Kikundi cha Umoja wa Wapanda Mikoko (UWAMIKO), Afri Craft pamoja na Timu ya Wataalam wa Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, wameendesha zoezi la upandaji wa miti ya mikoko katika maeneo yaliyoharibika, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zoezi hilo limefanyika tarehe 26 Agosti 2025 katika pwani ya Matuso, kata ya Masoko, ambapo jumla ya miche 4,339 ya mikoko imepandwa. Upandaji huo unalenga kurejesha uoto wa asili, kuimarisha kinga za pwani na kuendeleza urithi wa mazingira kwa vizazi vijavyo.
Afisa utawala TAMCO, Joel Fares amesema kuwa ushiriki wao katika zoezi hilo ni kuunga mkono jitihada za jamii katika utunzaji wa mazingira na kuhamasisha vizazi vijavyo kutunza rasilimali za asili.
Akitoa elimu juu ya umuhimu wa Mikoko moja ya wanakikundi cha UWAMIKO Ndg. Seif Najumwe ameeleza kuwa mikoko ni ngao ya asili ya pwani kwani husaidia kudhibiti mmomonyoko wa ardhi, kulinda fukwe dhidi ya mawimbi makubwa pamoja na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alibainisha kuwa mikoko ni makazi muhimu ya viumbe hai hususan samaki, kaa na ndege wa pwani, jambo linalochangia kuimarisha shughuli za uvuvi na kuendeleza rasilimali za bahari kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wao, Taasisi ya Afri Craft Tanzania waliwapongeza washiriki wote kwa mshikamano na mchango wao katika utunzaji wa mazingira, wakisisitiza kuwa mshirikiano wa kijamii na taasisi ni nguzo muhimu ya kufanikisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa