Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Ukaguzi huo umefanyika kama sehemu ya maandalizi ya Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Lindi, linalotarajiwa kufanyika tarehe 10 Julai 2025. Lengo kuu la jukwaa hilo ni kutathmini mchango wa mashirika katika ustawi wa jamii, kuainisha changamoto wanazokutana nazo, na kuimarisha ushirikiano kati yao na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, wataalamu hao walitembelea miradi ya mashirika ya MPINGO, TUJIWAKI na ACTIONAID, ambayo yanalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuboresha ustawi wa watoto, na kusaidia makundi maalum ndani ya jamii.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bi. Liliani Mganda, amesema
“Lengo letu si tu kufuatilia utekelezaji wa miradi, bali pia kuelewa namna mashirika haya yanavyochangia katika maendeleo ya wananchi, kubaini changamoto wanazokumbana nazo, na kuimarisha uratibu kati yao na Serikali.”
Mashirika yaliyotembelewa yaliwasilisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa miradi yao, ikiwemo ongezeko la uelewa wa kijinsia katika jamii, uimarishaji wa fursa za kiuchumi na ajira kwa wanawake na vijana, pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Hata hivyo, mashirika hayo pia yalibainisha changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wa miradi yao, zikiwemo ukosefu wa rasilimali za kifedha, uelewa mdogo wa jamii kuhusu miradi, na uhaba wa wataalamu wa kutekeleza shughuli za kiufundi.
Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali la Mkoa wa Lindi linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa ajili ya wadau wa maendeleo kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Lindi na taifa kwa ujumla
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa