Serikali Mkoani Lindi inatambua mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani humo na hivyo inaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi ili yaweze kujiendesha na kuwahudumia wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 10,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Hajjat Zainab Telack katika ufunguzi wa Kongamano la Mwaka la Mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani humo lililofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Manispaa ya Lindi.
Mhe. Mwanziva amepongeza NGO's zinazoendelea kufanya kazi ndani ya Mkoa wa Lindi ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan na ndio maana ipo Wizara ya Maendeleo ya Jamii inayosimamia vyema mashirika hayo kwa kuyatambua kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kama wabia muhimu katika maendeleo ya Taifa kwa kuhusisha wafadhili na watu walio katika hali mbalimbali.
Amesema kongamano hilo linaakisi tathmini ambayo serikali imekuwa inafanya kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kipindi cha miaka mitano ikilenga kuona mchango wa mashirika hayo kifursa ,changamoto na kupitia uendeshaji na shughuli zinazofanywa huku kupitia Sera ya Taifa ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya mwaka 2001 ikiendelea kuweka msingi wa uratibu wa mashirika hayo katika kujisajili nchini na kuainisha vyombo vya usimamizi.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii Bi. Francesca Herias amehimiza na kukumbusha wajumbe wa kongamano hilo kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa mashirika hayo ikiwemo kuwasilisha taarifa za mwaka sambamba na kuwa na miradi ambayo itawasaidia kujiendesha hata wanapokosa ufadhili.
Awali, Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Taifa Ndg.Gasper Makala ameeleza lengo la kongamono hilo licha ya kujadili changamoto bali kukumbushana wajibu na majukumu ya mashirika yasiyo ya kiserikali .
Na Msajili msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Lindi Ndg.Charles Kigahe, ametoa wito kwa mashirika yote ya mkoa wa Lindi ambayo yamesajiliwa kufanyakazi kulingana na mpango na malengo husika.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa