Shirika la Sea Sense limeendesha mafunzo ya siku nne kwa Viongozi wa Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kutoka Tarafa ya Pande, Wilaya ya Kilwa. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo wa viongozi hao katika usimamizi wa jamii kuhusu mifumo ya ikolojia ya baharini.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Tarehe 14 hadi 18Mei 2025 katika Shule ya Sekondari Matanda, Kata ya Lihimalyao, ambapo Mafunzo hayo yamejikita katika maeneo muhimu ya Usimamizi Shirikishi, Utawala Bora, Uongozi jumuishi unaozingatia usawa wa kijinsia, na ulinzi wa mazingira ya baharini. Washiriki walipata elimu ya kina kuhusu namna bora ya kushirikiana na jamii katika kulinda rasilimali za bahari na kuendeleza uvuvi endelevu.
Wakitoa mafunzo hayo Wawezeshaji kutoka Sea Sense walisisitiza umuhimu wa uongozi bora unaozingatia ushirikishwaji wa jamii nzima katika kulinda mazingira ya bahari ili kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho kinanufaika na rasilimali hizo.
Akizungumza moja ya Waliopatiwa Mafunzo hayo Bw.Said Mussa ametoa shukrani kwa Shirika la Sea Sense kwa kuwapatia Elimu ambayo itasaidia viongozi kuongeza Ufanisi katika uongozi wao hususani katika suala zima la kuzingatia utawala bora na ushirikishaji wa Wanananchi katika maamuzi katika utunzaji wa Rasilimali za uvuvi katika Tarafa hiyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa