Shirika lisilokuwa la Kiserikali lenye usajili namba OONGO/0506 liitwalo Sea Sense, limesema limeandaa mpango wa utunzaji wa Rasilimali za Bahari na Pwani katika Wilaya ya Kilwa hususani katika maeneo ya Kilwa Kusini.
Hayo yameelezwa wakati wa kikao cha pamoja baina ya Shirika hilo na Timu ya Menemeti ya Halmashauri ya Wilaya ya kilwa (CMT) kilichofanyika kwa lengo la kuwasilisha mipango ya miradi inayotekelezwa na Shirika hilo tarehe 11/02/2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa Masoko.
Katika wasilisho hilo Afisa Miradi kutoka Sea sense Ndg.Benard Kaitila amesema kuwa Shirika hilo linalenga kuhuisha na kuanzisha vikundi vya Usimamizi shirikishi (BMU) Kilwa Kusini, Kuzijengea uwezo BMU kwa mafunzo na Vitendea kazi, kuwezesha mchakato wa kuunda maeneo ya uvuvi ya Usimamizi wa Pamoja (CFMA), kuimarisha Usalama wa Chakula kwa kuwezesha matumizi endelevu ya mazao ya uvuvi na kuimarisha mashirikiano na wadau.
Kwa upande wake katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Yusuf Mwinyi ametoa pongezi kwa Sea Sense kwa kazi wanayoifanya katika utunzaji wa eneo la pwani Wilayani Kilwa, Aidha amewasihi kuitazama shughuli ya upandaji mikoko baharini kama shughuli ya kimkakati katika kutunza eneo la pwani lakini pia mikoko hiyo itatumika kupunguza nguvu ya mawimbi yanayokuja eneo la nchi kavu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Sea Sense Ndg. Gosbert Katunzi ameeleza kuwa shirika lao limejipanga vyema kutekeleza majukumu yao na kwa sasa wanatekeleza miradi hiyo kwa njia shirikishi kwa kuzingatia makundi maalumu katika jamii ambayo ni makundi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye mahitaji maalumu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa