Kilwa,
Mkuu wa mkoa wa lindi Mheshimiwa Godfrey Zambi ametembelea kiwanda cha Nitro Explosives Tanzania kilichopo katika kijiji cha Mavuji Wilayani Kilwa ambacho kinajihusisha na Uzalishaji wa Vilipuzi.
Akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Meneja Maendeleo Mapya ya Kampuni ya Nitro Explosives Tanzania Bw. Emmanuel Teekishe amesema Nitro Explosives Tanzania ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wake na wanatarajia kuanza uzalishaji Mwezi June 2019.
Bwana Teekishe amesema sanjari na ajira kwa vijana wa Kilwa, Halmashauri ya wilaya ya Kilwa itafaidika na kodi ambayo itakua ikilipwa baada ya kuanza kwa uzalishaji.
Pia amesema wakazi wa kijiji cha mavuji watafaidika na huduma za kijamii kama vile huduma ya maji safi na salama pamoja na kuboreshewa Zahanati ya Kijiji cha mavuji.
“Kuna baadhi ya mambo ambayo Kampuni itawafanyia wakazi wa Kijiji cha Mavuji baada ya kuanza uzalishaji. Tumepanga kuwachimbia Visima vya Maji safi na salama pamoja na kuboresha Zahanati ya mavuji, Kabla tulipanga kuwapelekekea huduma ya Maji kupitia visima ambavyo vimechimbwa hapa eneo la Kiwandani lakini kwa bahati mbaya ni Kisima kimoja tu kinatoa maji yasiyo na Chumvi na vilivyo baki vinatoa maji yenye Chumvi na kimoja hakitoi maji kabisa.
kutokana na sababu hiyo uongozi umeamua kwenda kuchimba Visima palepale Kijijini na Maji yanayopatikana hapa tutaendelea kuyatumia kwa matumizi mengine ya hapa kiwandani.
Kuhusu suala la Afya tumepanga kwenda kuboresha kile kituo kilichopo kwa sasa na kuongeza majengo yatakayo hitajika kutokana na uwezo wetu” alisema Teekishe.
Teekishe amesema kwa sasa kampuni ya Nitro Explosives Tanzania imetoa fursa kwa wakazi wa kijiji cha Mavuji kutumia gari ya kubebea wagonjwa muda wowote bila ya malipo.
“Kwa sasa kampuni yetu imetoa ruhusa kwa wanakijiji wa Mavuji kutumia gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) inayomilikiwa na kampuni hii bila malipo pindi itakapo hitajika, Madereva tunao na gari ipo kwahiyo muda wowote sisi tupo tayari kuwasaidiana nao” alihitimisha Teekishe.
Mkuu wa mkoa wa lindi Mh Godfrey Zambi (wa kwanza kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa kiwanda cha Nitro Explosives Tanzania alipotembelea kiwandani hapo June 26, wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya KIlwa Mheshimiwa Christopher Ngubiagai (PICHA :Ally Ruambo)
Kwa upande wake mkuuu wa mkoa wa Lindi Mh. Zambi ameushukuru uongozi wa Kampuni ya Nitro Explosives Tanzania kwa kuamua kuwekeza katika mkoa wa Lindi na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda
Aidha amewataka kujenga mahusiano mazuri kati yao na wananchi wanaowazunguka pamoja na serikali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa