Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, leo tarehe 01 Agosti 2025, amezindua rasmi Maonesho ya 12 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwa Kanda ya Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
Akihutubia wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Sawala amewataka wataalamu wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha wanatoa elimu stahiki na ya kisasa kwa wananchi, ili kuongeza maarifa na ubunifu katika shughuli zao za uzalishaji. Ameeleza kuwa maendeleo ya sekta hizi yanategemea kwa kiasi kikubwa uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia mpya, pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu na jamii.
Mkuu huyo wa Mkoa alitumia pia fursa hiyo kutembelea na kukagua mabanda mbalimbali ya maonesho, akianzia katika Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Akiwa hapo, alishuhudia bidhaa na teknolojia zinazotumika na kuzalishwa na wakulima, wafugaji na wavuvi, ikiwa ni ishara ya juhudi kubwa zinazofanywa katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijijini kupitia sekta za uzalishaji.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini ni jukwaa muhimu la mafunzo, maonesho ya teknolojia, ubunifu na fursa za kibiashara. Maonesho haya hufanyika kila mwaka yakijumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, na kwa mwaka huu yanafanyika kwa mara ya 12 mfululizo.
Kaulimbiu ya maonesho ya mwaka 2025 ni “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa