Katika kuendeleza dhamira ya uwajibikaji wa kijamii (CSR), Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) imekabidhi rasmi nyumba tano (two in one) kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, kwa ajili ya makazi ya walimu. Nyumba hizo zenye thamani ya TSh. Milioni 576,000,000/= zimejengwa katika maeneo ya Shule ya Msingi Ngea, Mitole, Ndende, Pande-Muungano, na Namatungutungu.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, iliyofanyika Tarehe 23 Julai 2025 Mhe. Nyundo ameipongeza kampuni ya PAET kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa katika kutatua changamoto za sekta ya afya na elimu wilayani Kilwa. "Tunawashukuru kwa kuendeleza heshima na sifa nzuri ya kampuni yenu kwa kutimiza majukumu ya uwajibikaji wa kijamii," amesema Mhe. Nyundo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi, hususan wazazi, kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi wa umma wanaopangiwa kazi katika maeneo yao, sambamba na kuwahimiza kuwapeleka watoto shule na kuwasimamia kupata elimu bora kwa maendeleo ya baadaye.
Kwa upande wake, Meneja wa Uwajibikaji wa Kijamii wa kampni ya PAET, Ndg. Andrew Kashangaki, amesema kila nyumba ina vyumba vitatu (master bedroom 1), jiko, sehemu ya kulia chakula (dining room), na tayari imeunganishwa na miundombinu ya umeme na maji.
Ndg. Kashangaki amebainisha kuwa kampuni hiyo inatarajia kukamilisha na kukabidhi nyumba nyingine sita zenye muundo unaofanana ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025, huku akieleza shukrani zake kwa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa ushirikiano mzuri wanaoupata.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Shija Lyella ameishukuru kampuni ya PAET kwa mchango wao mkubwa katika sekta ya Elimu na Afya wilayani Kilwa. Pia amewahimiza wazazi pamoja na walimu kuendelea kuhakikisha watoto wanapata chakula wawapo shuleni ili kuinua ufaulu na mazingira ya kujifunzia.
Makabidhiano hayo ni ushuhuda wa ushirikiano madhubuti kati ya serikali na sekta binafsi katika kuleta maendeleo kwa wananchi. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa inaendelea kuwakaribisha wadau mbalimbali kushiriki katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za kijamii
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa