Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe.Christopher Ngubiagai amewataka Wakala wa Maji vijijini Wilaya ya Kilwa(RUWASA) kutowabambikia wananchi bili za maji tofauti ya matuzmizi yao.
Mhe.Ngubiagai ameyasema hayo katika siku ya uzinduzi wa Mwongozo wa Jumuhia za huduma za maji ngazi ya jamii katika Wilaya ya Kilwa, Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa pamoja na kuwa wakala(RUWASA) anatakiwa kujiendesha bila kupata hasara lakini kwa sera za nchi na chini ya serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe.Dr.John Pombe Magufuli , bado maji ni sehemu ya huduma na si biashara na hivyo wananchi wote wana haki ya kupata maji safi na salama kwa gharama nafuu lakini pia bila kuletewa bili kubwa tofauti na matumizi yao. ‘Ndugu zangu , najua mna changamoto nyingi, lakini hili lipo ndani ya uwezo wenu, hakikisheni wananchi hao asilimia 62 walio kwenye mtandao wenu wa maji wanapata maji kwa uhakika na wanaridhika na huduma yenu’’ alisisitiza Mhe.Ngubiagai.
Kwa uapnde wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mh.Abuu Mjaka aliwataka wana jumuhia ngazi ya jamii waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia miradi ya maji kwa niaba ya wengine kufanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na kutoa nafasi kwa wakala kuwafikia wengine ambao mpaka sasa hawajafikiwa. ‘’Nimeambiwa hapa upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 59 na mjini ni aslimia 89 lakini bado uharibifu katika miundombinu hii iliopo ni mkubwa sana wakati nyie mpo na mnawafahamu wachache wanaohujumu huduma hizi’’ aliongeza Mhe.Mjaka.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa Mhandisi Ramadhani Mabula alimhakikishia mgeni rasmi kuwa wao kama Wakala wanaendelea kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa wakati na kwa uhakika huku akizitaja baadhi ya changamoto zinazowakumba kuwa ni pamoja na taasisi nyingi za serikali kuchelewa kuchelewa kulipa bili,ukataji wa bomba unaofanywa na wafugaji kwa lengo la kunywesha mifugo yao,Maji ya chumvi kuingilia miundombinu ambayo huko awali haikuwepo na kukatika kwa umeme mara kwa mara kunakopelekea mashine za kusukuma maji(Pampu) kuunguana kuharibika kabisa.
Mhandisi Mabula amesema pamoja na changamoto hizo lakini wameendelea kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii,kuomba Wizara ya Maji kulipa madeni ya wakandarasi kwa wakati pamoja na kuendelea na Tanesco ili kuhakikisha ukatikaji wa umeme mara kwa mara hauathiri mfumo wa maji.
Katika uzinduzi huo wadau kutoka sekta mbali mbali walialikwa lengo likiwa ni kuhakikisha mkiradi ya maji inayoanzishwa inakuwa endelevu bila kuhujumiwa kama ilivyokuwa huko nyuma ambapo wapo baaddhi ya wana jamii wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano wa taarifa za uharibifu unaotokea katika maeneo yao.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa