Kilwa,
Wananchi Wilayani Kilwa wame shauriwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya mwili ili kujiepusha na uwezekano wa kupata magonjwa yasiyoambukizwa.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai alipokua akihutubia wananchi waliojitokeza kufanya mazoezi ya viungo katika uwanja wa mpira wa miguu wa shule ya msingi Ukombozi mjini Kilwa Masoko.
Ngubiagai amesema mazoezi husaidia kupunguza uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa yasio ambukizwa kama vile Kisukari, Shinikizo la damu lakini pia humsaidia mtu kuweza kufikiri kwa haraka zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai (katikati) akiongoza zoezi la mwendo pole (jogging).
Aidha Mhe. Ngubiagai ameagiza wananchi kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafu na kuahidi kuwachukulia hatua wale wote ambao wataenda kinyume na agizo hilo.
“ kuna kikosi kazi kiumendwa kitapita mtaa kwa mtaa kukagua usafi wa mazingira, mazingira ambayo yatakayokutwa hayapo katika hali ya usafi wahusika watawajibishwa” alisistiza Ngubiagai.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa akishirikiana na wananchi kufanya usafi katika eneo la soko jipya baada ya mazoezi.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa Mhe. Abuu Mussa Mjaka amevitaka vikundi vya Mwendo pole (Jogging clubs) kushiriki katika shughuli za kijamii kama vile kufanya usafi katika maeneo tofauti tofauti ili kuiweka wilaya ya Kilwa katika hali ya usafi.
Akitoa mapendekezo yake mmoja wa wananchi waliojitokeza kufanya mazoezi Bw. Timami amesema itapendeza kama taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi zitaunda kundi (Jogging club) ambalo litakua likifanya mazoezi ya pamoja angalau mara mbili kwa wiki kwani mazoezi hujenga afya, umoja na mshikamano na kuahidi kutoa msada pindi utakapo hitajika.
Sanjari na mazoezi ya viungo lilifanyika zoezi la usafi katika eneo la soko jipya, zoezi ambalo liliongozwa na Mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, jeshi la polisi, Kivinje Jogging Club, Wanafunzi wa kidato cha tano na sita kutoka Kilwa Sekondari, wananchi pamoja na watumishi mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya kilwa kabla ya zoezi hilo kuhitimishwa kwa bonanza la Mpira wa wavu na Mpira wa Miguu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa