Mkuu wa Mkoa wa lindi Mhe. Godfrey Zambi ameiomba Wizara ya maliasili na utalii kuutazama Mkoa wa Lindi kwa Jicho Tatu katika sekta ya utalii.
Ombi hilo ameliwasilisha leo Oktoba 28 katika hitimisho la Tamasha la Ishirini na Tatu la Utamaduni wa Mtanzania ambalo kwa mwaka 2018 lilichagizwa na jamii ya watu wa Mkoa wa Lindi katika Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es salaam.
Zambi amesema Mkoa wa Lindi una Historia ya aina yake na Vivutio Vingi vya utalii lakini bado miundo mbinu ya kuvifikia vivutio hivyo siyo ya kuridhisha.
“Mhe. Naibu waziri Mkoa wa Lindi una vivutio vingi na vizuri sana kama wengi wetu hapa tunavyojua lakini bado miundo mbinu ya kuvifikia vivutio hivyo sio rafiki, kuna baadhi ya sehemu ukienda kwa kutumia Gari inakulazimu uliache mbali uanze kutembea kwa mguu” alisema Zambi
Pia Zambi amehoji juu ya Kumbukumbu ya Vita vya majimaji kufanyika Songea na si Kijiji cha Nandete wilayani Kilwa ambapo ndiyo chimbuko la Vita vya majimaji.
“Ukisoma historia utaona jinsi vita ya majimaji ilivyokuwa na jinsi waasisi walivyapambana na wakolini lakini tunashangaa maadhimisho ya kumbukumbu za vita ya majimaji kila mwaka yanafanyika Songea badala ya Kilwa ambako ndio chimbuko lake”
Akitolea ufafanuzi Hoja za Mkuu wa mkoa wa Lindi, Naibu waziri wa Maliasili na utalii (Mb) Mhe. Japhet Hasunga amesema serikali iko makini na inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya utalii na kuahidi kuendelea kuzitatua kadri iwezekanavyo.
“Ndugu yangu Zambi tunatambua changamoto ni nyingi na serikali iko macho kuhakikisha inaendelea kuboresha sekta ya Utalii kwa kutatua changamoto ambazo zinaenekana kuikabili sekta ya Maliasili na utalii, pia nikutoe wasiwasi kuhusu suala la Nandete tunafahamu kuwa huko ndiyo chimbuko la vita ya majimaji.
Pia Hasunga amewataka waandaaji wa matamashaya utamaduni kuendelea kuandaa matamasha mengine na kuitaka Mikoa ambayo haijafanya Tamasha la utamaduni kufanya na kufungua milango kwa mikoa iliyokwishafanya kufanya tena kama watahitaji.
Naibu waziri wa Maliasili na utalii (Mb) Mhe. Japhet Hasunga akipata maelekezo kutoka kwa Mtaalamu katika Banda la Makumbusho ya Taifa kuhusu Samaki ambaye alipotea miaka milioni sitini na tano iliyopita na kuonekana tena mwaka 2003 katika kijiji cha Songo Mnara wilayani kilwa (Picha: Ally Ruambo)
Aidha Mhe. Hasunga amewataka Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali ambavyo vinapatika katika Mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
“Msisubiri hadi sikukuu ndio muende huko panga muda wako nenda kale maisha, ukichukua likizo unaenda kafanye utalii, unakula maisha unarudi ukiwa na akili mpya ya kufanya kazi” alisema Hasunga
Katika hatua nyingine Naibu waziri ametoa maagizo kwa Mikoa yote ambayo haijajenga Nyumba za asili katika Kijiji cha Makumbusho kujenga Nyumba, Mkoa wa Lindi uchapishe Kitabu ambacho kitaelezea fursa zinazopatikana Mkoani humo na jinsi ya kuzifikia ili kiweze kutumika kama kitabu cha ziada kwa wanafunzi na watafiti mbalimbali, Mkoa wa Lindi ujenge makumbusho ambayo yatahifadhi historia na tamaduni za mkoa wa Lindi, Makumbusho kuandaa vitini vitavyoelezea sehemu na vifaa vya kujengea nyumba za asili katika kijiji cha makumbusho na kuvigawa Mikoani na taasisi ziendelee kujitokeza katika kuhifadhi na kutangaza tamaduni.
Awali akizungumza katika tamasha hilo Mkurugenzi mkuu wa makumbusho ya taifa Prof. Audax Mabula amemshukuru Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa ushirikiano aliouonyesha katika kuhakikisha tamasha la utamaduni wa Watu wa Lindi mwaka 2018 Linafanikiwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa