Kilwa,
Wananchi wa kata ya pande wamepongezwa kwa ushiriki wao katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Pande.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Zablon Bugingo na Watalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa walipotembelea kituoni hapo kukagua maendeleo ya mradi.
Bugingo amesema amefurahishwa na jinsi wananchi wanavyojitoa katika kusaidia shughuli za kila siku katika ujenzi wa kituo hicho.
“Nawapongeza wananchi wa kata ya pande kwa ushiriki wao katika mradi huu, msimamizi ameniambia kua misingi ya majengo haya imechimbwa na wananchi na haya Matofali yameletwa na wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao” alisema Bugingo.
Aidha amewataka wanakamati kufanya mikutano yao kwa wakati na kukabidhi muhtasari wa mambo waliyo adhimia ikiwemo orodha ya vifaa vya ujenzi wanavyotaka vinunuliwe ili viweze kufanyiwa mchakato wa manunuzi na kununuliwa mapema kabla ya vifaa vilivyopo eneo la mradi kumalizika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Zablon Bugingo (kati kati) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa Mafundi wanaoshiriki katika ujenzi katika Kituo cha Afya Pande baada ya kuwasili na timu ya Watalamu kukagua maendeleo ya Mradi(Picha : Ally Ruambo)
Nae mwenyekiti wa kijiji cha mikoma na Mjumbe wa kamati ya ujenzi kituo cha Afya Pande Bw. Shaweji Makame amesema wataendelea kuwahimiza wananchi juu ya ushiriki katika miradi ya kijamii.
“Tumejiwekea utaratibu wa kila kijiji kutoka Kata ya Pande kuja kujitolea katika Mradi huu na utaratibu unaendelea vizuri wananchi wanashiriki na sisi viongozi tutaendelea kutoa hamasa kwa wananchi waendelee kushiriki kwa wingi” alisema Makame.
Fundi akimwagia maji msingi wa moja ya majengo yanayojengwa katika Kituo cha Afya Pande kabla ya kupangwa Mawe na kumwagwa Zege (Picha : Ally Ruambo)
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Kilwa Bw. Sylvester Mashema amesema amefurahi kuona jamii inashiriki katika miradi ya maendeleo kwani hakuna maendeleo yanayoweza kuja bila ushirikiano.
Mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Pande utakapokamilika utaondoa adha ya wananchi wa kata ya pande na vijiji vya jirani kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya upasuaji na nyinginezo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa