Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndugu Renatus Mchau amewaasa watumishi wake kuendelea uchapa kazi katika maeneo yao mbali mbali ili kuleta tija kwa Halmashuari na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa ikiwa ni katika siku ya maadhimisho ya Wafanyakazi kote duniani ambapo kwa Mkoa wa Lindi siku hiyo iliadhimishwa katika viwanja vya Ilulu Katika Manispaa ya Lindi. ‘’Ndugu zangu, nyie mliopata zawadi ni sehemu ya watumishi wote, nawapongeza kwa kuwa kazi yenu imetambulika ila endeleeni kuchapa kazi Zaidi na zaidi’’ alisisitiza ndugu Mchau.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Kimkoa Mhe.Sara Chiwanga (Mkuu wa Wilaya ya Liwale) ambaye alimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Lindi Mhe.Godfrey Zambi. Mgeni Rasmi aliwataka watumishi wote kuendelea kuchapa kazi ili taifa liweze kupiga hatua kimaendeleo. ‘’Nimesikiliza hotuba yenu, yale yaliyo ndani ya uwezo wetu naahidi kuyafanyia kazi mara moja na yale ya Kitaifa nitayafikisha kwa wahusika’’ aliongeza Mhe.Chiwanga.
Mgeni rasmi aliwapongeza waajiri waliowazawadia watumishi wao zawadi zenje tija huku akiwasisitiza waajiri wengine pia kuhakikisha wanawatambua watumishi wao bora na kuwapongeza.
Kwa upande wa Wilaya ya Kilwa wafanyakazi Hodari kumi na moja walitambukuwa na kuzadiwa zawadi ya fedha taslimi laki tano (500,000) kila mmoja pamoja na cheti kutoka vyama vya wafanyakazi.
Watumishi waliotambuliwa ni kutoka idara mbali mbali ndani ya halmashauri kuanzia wale waliopo ofisi kuu za Halmashauri na wale kutoka sehemu mbali mbali za kutolea huduma kama vituo vya Afya , shuleni , vijiji pamoja na kata.
Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Bi.Jovita Buyobe aliwataja watumishi hao na nagfasi zao katika mabano kuwa ni Bi. Zuhurafu Mohamed Machenza(Katibu Muhtasi), Mohamed Litumbui (Mtendaji wa Kata ya Miguruwe),Bi.Tatu Kamtande(Mtendaji wa kata ya Kivinje) na Mwanahamii Omari (Mtendaji Kijiji ch Lihimalyao).
Idara ya Afya iliwakilishwa na watumishi watatu ambao ni Dr.Alfred Chinyeu(Kituo cha Afya Tingi) ,Bi.Getrude Nyaki (Muuguzi-Hospitali ya Kinyonga) na Bi.Anna Kapungu ambaye ni muhudumu wa Afya katika Zahanati ya Mkarango.
Watumishi wengine waliozawadiwa ni Said Pilla (Afisa Kilimo), Mwl.Selemani Msofe (Mkuu wa shule ya sekondari Kivinje), Mwl.Francis Siaga (Shule ya Msingi Nangorombe) na Mwl.Rabia Kilindo kutoka shule ya Nasaya.
Bi Buyobe alieleza kuwa upatikanaji wa watumishi hao umezingatia vigezi vingi ikiwa ni pamoja na watumishi kupigiwa kura za wazi na za siri, mazingira yao ya utumishi lakini kikubwa wamepatikana kutokana na uchapakazi wao.
Mmoja wa viongozi wa chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa(TALGWU) ndugu Hajji Limba alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwatambua wafanyakazi hodari na kuwazawadia kwa wakati. ‘’Nadhani mmeona baadhi ya waajiri wamekuja pale na ahadi lakini sisi Mkurugenzi wetu Bw.Mchau alibeba kabisa fedha taslimu na kila mmoja amepata kile alichostahili, sisi tuna Mkurugnzi Jembe na tunamuahidi tutaendelea kuchapa kazi’’ alimalizia Ndugu Limba.
Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitafa yamefanyika katika Viwanja vya CCM –Kirumba jijini Mwanza ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa