Mkoa wa Lindi unaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha unapunguza matatizo yatokanayo na lishe duniMkoa ikiwemo udumavu, ukondefu,uzito uliozidi,lishe duni, kiriba tumbo na ukosefu wa damu kwa wanawake walio katika umri wa uzazi.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala Msaidizi Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Lindi Dkt. Kheri Kagya alipokua anamuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary katika Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji yaliyofanyika kimkoa katika Kituo cha Afya Tingi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ambapo ameeleza kuwa Mkoa umechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wanakabiliana na hali hiyo ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo redio na maadhimisho ya siku ya afya na lishe kwa ngazi za vijiji na mitaa.
"Tunaendelea kusisitiza wanajamii kuhusu uzingatiaji wa elimu ya ulaji unaofaa unaohusisha makundi yote sita ya vyakula, sambamba na uzingatiaji wa lishe ya watoto wadogo na wachanga ikiwemo unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo na kuendelea kuwanyonyesha watoto hadi wanapofika umri wa miaka miwili tukizingatia kuwa lishe bora katika siku 1000 za mwanzo ni muhimu kwa afya ya mama na ukuaji wa mtoto na kuzuia madhara yatokanayo na udumavu yanayoweza kuathiri maendeleo ya ukuaji na afya ya akili ya mtoto" ameeleza Dkt. Kagya.
Aidha, Dkt. Kagya amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuzingatia unyonyesha wa watoto kwa muda wa miaka miwili ambapo ameeleza kuwa maziwa ya mama ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa ubongo wa mtoto, kukinga mtoto dhidi ya maradhi pia yana gharama nafuu na upatikanaji rahisi kuliko maziwa mengine.
Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji huadhimishwa kila mwaka kianzia tarehe 1 hadi 7 ya mwezi Agosti ambapo kwa mwaka huu yamepambwa na kauli mbiu isemayo " Tatua Changamoto, Saidia Unyonyeshaji kwa Watoto" ikiwa imelenga kutoa elimu na kujazia mapungufu yaliyopo ndani ya jamii kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto ikiwemo kipindi cha dharura na majanga.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa