Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini Ndg. Shija Lyella amefungua rasmi mafunzo ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata kwa majimbo ya Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini. Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa Masoko, kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 04 -06 Agosti 2025.
Mafunzo hayo yanahusisha washiriki 46 kutoka kata 23 za Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, yakilenga kuwaandaa kikamilifu kwa ajili ya kusimamia uchaguzi mkuu kwa ufanisi, kwa mujibu wa Katiba, sheria na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Ndg. Lyella amewataka washiriki wa mafunzo kutumia ipasavyo muda wa mafunzo kwa kusikiliza, kuuliza maswali na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi.
Katika hatua ya kuimarisha maadili na uaminifu wa wasimamizi wa uchaguzi, washiriki wote wamekula viapo viwili muhimu mbele ya Mhe. Beatrice C. Misiagate, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kilwa Masoko. Viapo hivyo ni kiapo cha kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa, pamoja na kiapo cha kutunza siri.
Mafunzo haya yanatarajiwa kujenga uwezo wa pamoja kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhusu wajibu wao, taratibu za kisheria, mazingira ya kazi, na mbinu sahihi za kudhibiti changamoto katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa