Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu Jimbo ya Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini, Ndg. Shija Lyella, leo tarehe 06 Agosti 2025 ametamatisha rasmi mafunzo ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata. Mafunzo haya yamefanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC), Kilwa Masoko na yamehusisha jumla ya kata 23 kutoka katika majimbo hayo mawili.
Kwa muda wa siku tatu, washiriki wa mafunzo hayo wamepitia mada mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo katika kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo na maadili ya uchaguzi nchini. Mafunzo yamejikita zaidi katika kuimarisha uelewa wa kiutendaji, kusimamia haki na kuhakikisha uwazi katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi.
Ndg. Lyella, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, amewapongeza wasimamizi kwa ushiriki mzuri na umakini waliouonesha katika kipindi chote cha mafunzo. Amesisitiza kuwa mafanikio ya uchaguzi hutegemea kwa kiasi kikubwa utayari wa wasimamizi wa uchaguzi katika kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu, uaminifu na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Pamoja na mafunzo, wasimamizi hao wamepokea vifaa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao katika kata wanazohudumu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Aidha, Ndg. Lyella amewakumbusha wasimamizi kuhusu viapo vya uaminifu walivyokula akisisitiza kuwa ni viapo vya kisheria vinavyowataka kutunza siri, kuwa waadilifu na kutotanguliza maslahi binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa