KUMBUKIZI YA MIAKA 114 YA MAJIMAJI YAFANA KIPATIMU
Maadhimisho ya miaka 114 tangu kumalizika kwa vita vya majimaji vilivyopiganwa kati ya waafrika wa kusini mwa Tanganyika na Wajerumani yamefanyika katika kijiji Nandete kata ya Kipatimu Wilayani Kilwa.
Maadhimisho hayo ambayo kwa miaka kadhaa yamekuwa yakifanyika nje ya Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi yalihudhuriwa na wanannchi wengi wakiwemo wazee wa maeneo husika ambao walitoa historian a kueleza kuwa vita vya Maji maji chimbuko lake ni Kata ya Kipatimu Wilaya ya Kilwa na si vinginevyo kama ambavyo baadhi watu wanavyoeleza na kuelewa.
Mgeni rasmi katika kumbukizi hizo Mhe. Christopher Ngubiagai ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kilwa aliwapongeza wazee wa vijiji vinavyoznguka eneo hilo kwa kuendelea kutunza historia pamoja na mnara wa kumbukumbu wa vita hivyo iliyowekwa na Rais wa awamu ya nne Mhe.Dr.Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2010 katika kijiji cha Nandete katika kata ya Kipatimu. Mnara huo wenye majina ya wahanga wa vita hivyo ni sehemu muhimu ya historia ambapo wadadisi mbalimbali wa mambo ya kale hufika katika eneo hilo kupata historia.
Akiongea kwenye maadhimisho hayo, Mhe.Ngubiagai aliwapongeza wazee wa eneo hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutangaza historia hiyo kwa faida wakazi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla.
Mmoja wa wazee wa Vijiji hivyo ambaye pia ni mwana historia mzee Batoli Mweo alitoa historia ya chanzo cha vita hivyo kuwa kitendo cha wakoloni wa Kijerumani waliofika katika eneo hilo kulazimisha kilimo cha zao la Pamba jambo ambalo liliwakasirisha wazee hao na kuamua kung’oa pamba na ndiyo ikawa chanzo cha vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.
Katika kata ya Kipatimu pia kuna vivutio vingine kama mapango ya Nang’oma katika kijiji cha Nandembo ambayo yanasemekana kwa makubwa Zaidi barani Afrika yakiwa na urefu wa Zaidi ya kilomita saba ambacho hakijatangazwa kiasi cha kutosha. Mzee Batoli anaeleza kuwa katika mapango hayo ambayo yanaaminika kutumika kama maficho ya waafika katika kipindi cha vita hivyo pamoja na kiongozi wao Kinjekitile Ngwale kuna kuna vivutio vingi na wageni kadhaa wamekuwa wakifika kujifunza ingawa ni kwa kiasi kidogo jambo ambalo linawanyima mapato lakini pia fursa ya kujulikana duniani kote tofauti na mapango kama ya Amboni mkoani Tanga ambayo ni madogo Zaidi ukilinganisha na mapango ya Nang’oma.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na sherehe za kijadi pamoja na uwekaji shada la maua na silaha za jadi zilizowekwa na viongozi wa serikali, viongozi wa jadi na viongozi wa dini.
Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na Mbunge wa Kilwa Kaskazini Mhe.Vedasto Ngombale,kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Adv.Godfrey Jafari, waheshimiwa madiwani pamoja na wananchi kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa