Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imeshiriki kwa mafanikio makubwa katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji (LINDI MINING EXPO 2025), ambayo yamewaleta pamoja wadau wa maendeleo, wawekezaji na wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa wa Lindi. Lengo kuu la ushiriki huo ni kutangaza kwa upana fursa mbalimbali za kiuchumi na utajiri wa maliasili zinazopatikana ndani ya Wilaya ya Kilwa.
Kupitia banda maalum lililoandaliwa kwa umahiri na kitaalamu, Halmashauri ya Kilwa imeonesha kwa vitendo ukubwa wa fursa zilizopo kwa ajili ya uwekezaji endelevu. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na uwepo wa madini ya viwandani na vito katika maeneo mbalimbali; uchumi wa bluu unaojumuisha uvuvi wa kisasa, ufugaji wa samaki na uzalishaji wa mazao ya baharini kama mwani; kilimo cha mazao ya biashara ikiwemo korosho, mbaazi na ufuta kwa kutumia ardhi yenye rutuba; pamoja na fursa za uvuvi wa kisasa na uanzishaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi.
Pia, Wilaya ya Kilwa imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii wa kihistoria kama Kilwa Kisiwani na Songo Mnara pamoja na visiwa vyenye mandhari ya kuvutia; Bandari ya Kilwa Masoko ambayo ina nafasi kubwa ya kupanuliwa kwa ajili ya shughuli za biashara na usafirishaji; misitu ya asili na ya kupandwa kwa matumizi ya mbao na miradi ya uhifadhi wa mazingira; na visiwa vinavyofaa kwa uwekezaji katika sekta ya hoteli, mapumziko na utalii wa kiikolojia.
Aidha, kupitia maonesho haya, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika maendeleo ya taifa, ikiwemo kuhimiza ushiriki mpana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni.
"Madini na Uwekezaji Fursa ya Kiuchumi Lindi.
Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025."
Ushiriki wa Halmashauri ya Kilwa katika maonesho haya ni sehemu ya mkakati mpana wa kuitangaza Wilaya hiyo kama kitovu cha fursa za kiuchumi, chenye mazingira rafiki kwa uwekezaji, huku ikilenga kukuza ajira, uchumi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya kijamii kwa ujumla.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa