Katika juhudi za kuimarisha Afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao yake, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imepokea jumla ya dozi 79,000 za chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa ng’ombe na dozi 204,000 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Sotoka kwa mbuzi na kondoo, chanjo hizo zimetolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo za ruzuku kwa mwaka wa fedha 2024/2025, na zimepokelewa rasmi kupitia kitengo cha Mifugo cha Wilaya ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya chanjo hizo, Mkuu wa kitengo cha Mifugo wilayani Kilwa, Ndg. Sifael Mwanyhesi, amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia wafugaji kwa kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma za chanjo, pia Ndg, Mwanyhesi amesema chanjo hizo zitatolewa kwa ruzuku ambapo kila ng’ombe atachanjwa kwa shilingi 500 tu badala ya shilingi 1,000, huku mbuzi na kondoo wakichanjwa kwa shilingi 300 badala ya shilingi 600.
“Hii ni fursa adhimu kwa wafugaji wetu. Kupitia bei hii ya ruzuku, tunatarajia kuona ushiriki mkubwa kutoka kwa jamii, hii itasaidia kupunguza vifo vya mifugo, kuongeza usalama wa chakula na kukuza uchumi wa kaya zinazotegemea ufugaji,” amesema Ndg. Mwanyhesi.
Ndg. Mwanyhesi. Ameeleza kuwa serikali inalenga kuchanja angalau asilimia 70% ya mifugo nchini ili kufikia viwango vya kimataifa vya afya ya mifugo, hatua itakayowezesha mifugo ya Tanzania kushindana kwenye soko la kimataifa kwa ubora.
Aidha, ametoa wito kwa wafugaji wote wilayani Kilwa kujiandaa kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo ya chanjo, akisisitiza kuwa Afya bora ya mifugo ni msingi wa ustawi wa jamii nzima.
Chanjo hizo zinatarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kilwa kupitia ratiba maalum itakayopangwa na wataalamu wa mifugo wa halmashauri hiyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa