Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imepokea pikipiki 11 kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuimarisha huduma za ugani na utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo kwa Maafisa Mifugo wa ngazi ya kata, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ndg. Shija Lyella, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwapatia pikipiki hizo ambazo zitasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za ugani wilayani Kilwa.
Aidha, Ndg. Lyella aliwataka Maafisa Mifugo kuhakikisha matumizi sahihi ya pikipiki hizo kwa kazi zilizokusudiwa. “Pikipiki hizi zisitumike kama bodaboda, bali zitumike kwa ajili ya kutoa huduma za mifugo,” alisisitiza.
Pikipiki hizo ni sehemu ya mgao wa kitaifa wa pikipiki 700 zilizotolewa kwa Maafisa Mifugo ngazi ya wilaya na kata nchini, ikiwa ni mkakati wa Serikali kuwafikia wafugaji walioko vijijini kwa urahisi zaidi na kutoa huduma bora za afya ya mifugo.
Katika mgao huu, pikipiki zimegawiwa kwa maeneo ya Somanga (2), Kikole (1), Likawage (1), Mitole (1), Mandawa (1), Njinjo (1), Kivinje (2), Makao Makuu ya Idara ya Mifugo (1), na Mratibu wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi (1).
Kupatikana kwa vitendea kazi hivi ni hatua muhimu katika utekelezaji wa kampeni iliyoanzishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 16 Juni 2025, Bariadi–Simiyu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa