Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Hemed S. Magaro, akiambatana na baadhi ya Wataalamu kutoka Halmashauri hiyo pamoja na viongozi wa Mtandao wa BMU (Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Bahari) na viongozi wa BMU wamefanya ziara ya kujifunza katika Halmashauri ya wilaya ya Pangani mbinu za ukusanyaji wa mapato ya baharini kupitia BMU, ikiwa Pangani ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na bahari kwa kutumia BMU.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo mwekahazina wa BMU Kipumbi Pangani, Ndg. Mohamed Ally Juma amesema, “Siri ya mafanikio yetu imejikita kwenye ushirikiano wa karibu kati ya Halmashauri na BMU kupitia mikataba rasmi. Mikataba hii imeweka uwazi wa majukumu na mapato, huku BMU ikipatiwa asilimia 10 ya mapato waliyokusanya kama motisha ya kazi zao. Tunashauri Kilwa kuanzisha mfumo kama huu ambao sio tu unaongeza mapato ya halmashauri, bali pia unaongeza morali kwa BMU.”
“Ni muhimu pia kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na BMU, kutoa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa mapato, pamoja na kuhakikisha stahiki za BMU zinapatikana kwa wakati. Hili linaongeza imani na kujituma kwa vitendo.”
Ziara hiyo pia imelenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Halmashauri, BMU na wavuvi ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinatumika kwa tija na zinachangia kikamilifu mapato ya Serikali.
Kilwa inaendelea kujifunza na kuboresha mifumo yake kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi na halmashauri kupitia sekta ya uvuvi na bahari.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa