Magofu, ndio wazo kubwa ambalo limekua likitawala vichwani mwa watu wengi pindi wasikiapo jina la mji adhimu huu ambao umeendelea kujizolea umaarufu ndani na nje ya nchi kila uchao.
Idadi kubwa ya watu wamekua wakisafiri kutoka nchi na mikoa mbalimbali kuja kujionea kwa macho sifa ambazo wamekua wakizisoma na kuzisikia katika vitabu na mitandao mbalimbali.
Sanjari na shauku ya kujionea yale ambayo wamekua wakiyasikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari lakini utulivu , ukarimu na busara za wenyeji na wakazi wa mji huu ndio sababu nyingine kubwa ambayo inawafanya watu kutoka nchi mbalimbali kuendelea kumiminika katika mji huu adhimu katika historia ya Tanzania na Pwani ya afrika mashariki kwa ujumla.
Hii ndio Kilwa, Wilaya ambayo mwenyezi mungu ameitunuku tunu kubwa na ya aina yake ukilinganisha na miji mingine ambayo inapatikana katika mgongo wa dunia.
Wajihi wake unatosha kuthibitisha kauli hii kwani umepambwa ukapambika kwa ardhi yenye rutuba ambayo ukubali kumea mazao ya aina mbalimbali, mito, milima, mabonde, mapango, maliasili pamoja na fukwe ndefu za bahari zenye kupendeza.
Kwa miaka mingi kilwa imekua ikijizolea umaarufu kwa uwepo wa vivutio ambavyo vimekua vikiteka hisia watalii ambao wamethubutu kuitembelea kilwa. Uwepo wa Magofu ambayo yalikua yakitumika na utawala wa kisultani katika karne ya 14 hadi 19 umezidi kuipamba na kuiongezea sifa wilaya hii.
Wengi wao wamekua wakiyajua magofu ya msikiti wa karne hizo ambao ulikuwa mkubwa na maarufu kuliko yote katika Afrika ya Mshariki, ngome ya Wareno,Husuni kubwa na ndogo ambayo yanapatikana kilwa kisiwani licha ya kua kuna magofu mengine mengi katika Mji wa kilwa kivinje ,songo mnara na kwengineko labda kwa kua yamekua yakitangazwa sana licha ya kua na vivutio vingi zaidi ya hivi ambavyo vimekua vikitawala midomoni na masikioni mwa wengi wetu.
Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu ni kua katika nyanja ya utalii Kilwa inazaidi ya magofu, ingawaje wengi wamekua wakidhani kilwa hakuna vivutio vingine zaidi ya magofu, ukiwa wilayani kilwa unaweza kutembelea vivutio na kufanya mambo mengi ambayo yatakuacha ukistaajabu.
Mapango,
kilwa ina mapango ya asili yajulikanayo kwa jina la mapango ya Nong’oma, mapango ya asili ambayo yapo enzi na enzi katika kijiji cha Nandete, kata ya Kipatimu wilaya ya kilwa. Hiki ni kivutio kizuri ambacho watalii wa ndani na nje wanaweza kutembelea na kujifunza mengi.
Mto Nyange,
Umaarufuwa mto huu ni kuwa na viboko wengi ambao wanatabia tofauti na Viboko wengine ambao wamezoeleka. Viboko hawa wana tabia ya kucheka, kufanya yale wanayoamrishwa kufanya na kujitokeza pindi wanapohitajika. Wanyama hawa maisha yao kwa asilimia mkubwa huishi majini kuliko nchi kavu, pua zao macho na masikio yapo juu ya fuvu la kichwa hali ambayo humuwezesha kuzamisha sehemu kubwa ya mwili wake katika maji au matope.
Hifadhi ya Selous,
Ni hifadhi ambayo inashika usukani miongoni mwa hifadhi zinazopatikana nchini Tanzania ikiwa na eneo la Km 54,600 na ni miongoni mwa hifadhi mkubwa duniani .Kutokana na ukubwa wake hifadhi hii imegusa mikoa kadhaa ikiwemo Pwani, Morogoro,Lindi, Mtwara, na Ruvuma. Ukiwa kilwa anauwezo wa kufika katika hifadhi hii na kujionea wajihi wake ulivyo pambwa kwa wanyama wa aina mbalmbali.
Fukwe,
ukiwa kilwa uneweza kutembelea fukwe kadhaa ambazo zitakufanya uburudike na kukuacha kinywa wazi ukistaajabu kwa jinsi zilivyo ndefu na za kuvutia. Kuna fukwe nyingi miongoni mwa hizo kuna fukwe ambazo ni maarufu kama Jimbiza (Jb) na Masoko Pwani.
Hoteli za kitalii,
hoteli za kitalii ni vivutio vingine ambavyo vinapamba na kufanya wajihi wa fukwe za bahari ziwe na muonekano murua kwa watembeleaji. Ukiwa kilwa unaweza kupata huduma za chakula na malazi katika hoteli mbalimbali za kitalii ambazo zimejengwa kwa mitindo tofauti tofauti.
Mikoko,
Pwani ya Kilwa ina misitu ya miti ya mikoko ambayo ilitumika katika ujenzi wa nyumba Kilwa. Baadhi ya majengo yaliyojengwa na mikoko kaika karne ya 14 hadi 19 bado zingine zinatumika. Miti ya mikoko inasifika kua ni miti imara ambayo ina uwezo wa kuhimiri mashambulizi ya wadudu waharibifu kama nchwa.
Kama hio haitoshi ukiwa kilwa una uwezo wa kuukongo moyo kwa kufanya michezo pamoja na shughuli nyingine ambazo ni nadra kupatikana sehemu nyingine
Sports fishing,
hii ni aina ya uvuvi ambao hufanywa kwa ajili ya burudani tu na si kwa ajili ya biashara au kwa ajili ya chakula. Aina hii ya uvuvi samaki wakubwa uvuliwa kwa kutumia ndoano kisha mvuvi awaangalia au kupiga nao picha na kuwaachia wakiwa hai, Samaki wanaovuliwa ni papa, samsuli, jodari, chewa na songoro.
Kuogelea,
Maji ya Pwani ya kilwa ni mazuri kwa kupiga mbizi. Maji haya hajaharibiwa na shughuli za kibinadamu mtu anaweza kuona mpaka mita 30 akiwa amepiga mbizi.mamia ya watalii kutoka nchi za nje na wakazi wa kilwa wamekua wakiogelea na kupiga mbizi.
Uwindaji, Kuna maeneo ya mapori huria yaliyotengwa kilwa ya kuwindia wanyamaori yanayojulikana kama ‘hunting block’s. Hivi sasa mapori hayo watalii huwinda wakati wa msimu.
“kwenye miti hakuna wajenzi” ndio msemo unaoweza kusadifu maudhui yanayoikumba wilaya ya kilwa katika ustawi wa sekta ya utalii. Kilwa ina kabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya utalii ukilinganisha na sehemu zingine ambazo zimekua zikiendesha shughuli za utalii.
Miundo mbinu katika kurahisisha kufika katika vituo bado haikidhi haja, mfano mzuri ni ukosefu wa boti ziendazo kasi ambazo zinaweza kufanya safari iliokua ya masaa mawili kupungua mpaka lisaa. Lakini pia njia za kuelekea sehemu za vivutio wakati wa mvua zimekua na changamoto ya kupitika kwa shida kama sio kupitika kabisa.
Pia ukosefu wa Hoteli za kitalii zenye hadhi kubwa imekua changamoto ambayo inaitafuna sekta ya utalii kilwa, hoteli zilizopo bado hazijafikia kiwango cha ushindani na hoteli zingine ambazo zinatoa huduma kwa watalii.
Elimu juu ya vivutio pia ni changamoto nyingine ambayo ipo miongoni mwa watanzania haswa wazawa wa kilwa, watanzania wengi wamekua hawana ufahamu juu ya vivutio vinavyopatikan a kilwa ukifananisha na ufahamu walio nao juu ya vivutio vingine kama vile mlima Kilimanjaro na hifadhi mbalimbali.
Vyombo vya habari, navyo kwa namna moja wamekua wakiangazia vivutio ambavyo ni maarufu, na inapotokea inaangazia kilwa hawaingii ndani huko kama kwenye mapango, zaidi ya magofu hali ambayo inawafanya watu wengi kuwa na mawazo butu juu ya kilwa.
uwepo wa vivutio hivi unafanya kuwepo kwa hekta 844.24 ambazo zinaweza tumika kwa fursa za uwekezaji, hivyo ni fursa kwa mashirika , watu binafsi, makampuni kutoka ndani na nje ya nchi kutumia changamoto hizo kuja kuwekeaza kilwa katika sekta ya utalii ili kuongeza ajira, pato la wilaya na taifa kwa ujumla.
#KilwaTourism
#KilwaDream
#Selous
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa