Maonesho makubwa ya Madini na Fursa za Uwekezaji yamezinduliwa rasmi Tarehe 11 Juni 2025 katika Viwanja vya Madini Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi, yakikusanya wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka sekta ya umma na binafsi.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa washiriki wakuu katika maonesho hayo, ikijivunia kuwasilisha fursa lukuki zinazopatikana ndani ya wilaya ya Kilwa yenye historia, rasilimali na mazingira ya kipekee yanayovutia uwekezaji wa aina mbalimbali.
Katika banda la Halmashauri ya Kilwa, wageni na wawekezaji wanapata fursa ya kujifunza kwa undani kuhusu maeneo mbalimbali ya uwekezaji kama vile:
Sekta ya Madini – Ikijumuisha maeneo yenye utajiri wa madini kama chumvi na chokaa.
Kilimo na Uvuvi – Fursa za uzalishaji wa mazao ya kimkakati na uvuvi endelevu wa bahari na maji baridi.
Utalii – Ikijumuisha vivutio vya kihistoria kama mji wa kale wa Kilwa Kisiwani,fukwe safi, na mandhari ya kuvutia ya bahari.
Misitu, Viwanda na Biashara – Uwekezaji katika bidhaa za mazao ya misitu, usindikaji wa mazao ya kilimo na ufunguzi wa viwanda vidogo na vya kati.
Uwekezaji wa moja kwa moja – Ikijumuisha maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Maonesho haya yanalenga kukuza uelewa wa wananchi kuhusu rasilimali zilizopo na kuwavutia wawekezaji kuchangamkia fursa mbalimbali zinazoweza kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na taifa kwa ujumla.
Karibu sana katika Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili uweze kutambua, gundua na wekeza kwa maendeleo endelevu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa