Kilwa, Lindi – Julai 4, 2025
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, ametoa wito kwa wafugaji wilayani Kilwa kushiriki kikamilifu katika juhudi za serikali za kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazoikumba mifugo yao.
Bi. Meena ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo uliofanyika katika kijiji cha Matandu, kata ya Kivinje. Lengo ni kutoa chanjo dhidi ya magonjwa hatari kwa mifugo ikiwemo Mdondo (Newcastle Disease), Mapafu ya Ng’ombe (CBPP) na Sotoka kwa Mbuzi na Kondoo.
“Kama ambavyo mkulima hawezi kuzalisha mwaka mzima bila chanzo thabiti cha maji, vivyo hivyo mfugaji hawezi kuwa na mifugo yenye afya bila miundombinu ya msingi kama vile visima na vituo vya huduma za mifugo. Ni wakati wa wafugaji wetu kushiriki kwa dhati katika uboreshaji wa huduma hizi,” amesema Bi. Meena.
Aidha, ameeleza kuwa serikali iko tayari kusaidia maeneo yenye changamoto kubwa, lakini masuala madogo yanayohitaji nguvu kazi au rasilimali kidogo yanapaswa kushughulikiwa kwa ushirikiano wa moja kwa moja kati ya jamii ya wafugaji na serikali za mitaa. Pia alibainisha kuwa chanjo kwa kuku zitatolewa bila malipo, lakini ng’ombe, mbuzi na kondoo mfugaji atachangia nusu ya gharama za chanjo husika. Pia amehimiza usimamizi madhubuti na ufuatiliaji wa wataalamu wa mifugo ili kuhakikisha chanjo zinatolewa kama ilivyokusudiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Ndg. Yusuf Mwinyi, amewataka wafugaji kuchangamkia fursa ya chanjo za ruzuku ili kulinda mifugo dhidi ya magonjwa hatari yanayoathiri uzalishaji na soko la mifugo.
Naye Daktari wa Mifugo kutoka Halmasahuri hiyo Dkt. Nyalekwa Mashimo ameeleza kuwa tayari halmashauri imepokea jumla ya dozi 300,000 za chanjo ya mdondo kwa kuku, dozi 79,000 za CBPP kwa ng’ombe, na dozi 204,000 za chanjo ya sotoka kwa mbuzi na kondoo. Alibainisha kuwa tangu tarehe 30 Juni 2025 hadi sasa Halmasauri imefanikiwa kutoa chanjo 30,000 kwa kuku sawa na asilimia 10 ya dozi iliyotolewa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa