Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Mohamed Nyundo ameongoza Mkutano Maalum wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Kilwa kwa lengo la kujadili Mapendekezo ya kugawa Majimbo Mawili ya Uchaguzi ambayo ni Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini ili kupata Jimbo Jipya la Uchaguzi la Kilwa Mashariki. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Sultani uliopo Kilwa Masoko Tarehe 11/03/2025.
Mapendekezo ya Muundo wa Majimbo hayo ni kama ifuatavyo; Jimbo la Kilwa Kaskazini linapendekezwa kuwa na Kata ya Kipatimu, Kandawale, Chumo, Namayuni, Kibata, Mingumbi, Kinjumbi, na Somanga. Jimbo la Kilwa Kusini linapendekezwa kuwa na Kata ya Pande, Lihimalyao, Mandawa, Kiranjeranje, Nanjirinji, Likawage, Njinjo na Miguruwe na Jimbo la Kilwa Mashariki linapendekezwa kuwa na Kata ya Songosongo, Masoko, kivinje, Tingi, Miteja, Kikole na Mitole.
Baadhi ya Sifa za majimbo hayo ni kama ifuatavyo. Jimbo la Kilwa Kaskazini litakuwa na wastani wa Idadi ya Watu 94, 845 na Ukubwa wa eneo ni Kilometa za Mraba 2,074.63. Jimbo la Kilwa Kusini litakuwa na wastani wa Idadi ya Watu 112,682 na Ukubwa wa Eneo ni Kilometa za Mraba 8,959.68 na Jimbo la Kilwa Mashariki litakuwa na Wastani wa Idadi ya Watu 90,149 na Ukubwa wa Eneo ni Kilometa za Mraba 2,313.18. Takwimu za Idadi ya Watu ni kwa Mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za Mwaka 2022.
Pamoja na Kupokea Maoni na Ushauri kutoka kwa Wajumbe wa Kikao Hicho Mhe. Nyundo amewashukuru wajumbe wote kwa kuitikia wito na kufika kwa wingi ili kuchangia mawazo yao kwa ajili ya Maendeleo ya Wilaya ya Kilwa. Aidha Mhe. Nyundo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Fursa Hii kwa Watanzania Ili kuongeza wigo wa ushirikishwaji wa wananchi kupitia mwakilishi wao, Kuongeza Uwajibikaji kwa Viongozi kwa kupunguza Ukubwa wa Majimbo na kuongeza Usawa katika Mgawanyo wa Rasilimali na Utoaji wa Huduma za Kijamii.
Ikumbukwe kuwa ugawaji wa Majimbo umezingatia Vigezo vyote vya Ugawaji wa Majimbo kama inavyopendekezwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa