Mkuu wa Wilaya ya Kilwa na Mwenyekiyiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Mhe. Mohamed Nyundo amefunga rasmi mafunzo ya miezi minne (4) kwa askari wapatao 131 wa awamu ya 16 ya Mafunzo ya jeshi la Akiba katika kata ya Somanga Wilayani humo leo tarehe 08 Novemba 2024.
Katika hafla ya kufunga mafunzo hayo Mhe. Nyundo amewapongeza wakufunzi wa askari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya. “Ninaona vijana wana utofauti mkubwa ukilinganisha na kipindi wanaanza mafunzo haya, wamebadilika kutoka kuwa goigoi, vijana wasio na nidhamu, vijana wasio na utayari wa kufanya kazi na sasa wamekuwa vijana wakakamavu, wenye utimamu wa akili pamoja na utayari wa kulitumikia taifa lao” Amesema DC Nyundo.
Kwa upande wake Mshauri wa jeshi la Akiba Wilaya ya Kilwa Luteni Kanali Philipo William Mwangatwa amesema mafunzo hayo yalianza rasmi 01/07/2024 yakiwa na vijana wapatao 149 kati yao wanaume wakiwa 107 na wanawake wakiwa 42 na leo tarehe 08/11/2024 wamehitimu askari wapatao 131 kati yao wanaume wakiwa 94 na wanawake wakiwa 37.
Katika mafunzo hayo askari wamepata ujuzi mbalimbali ikiwemo ujanja wa porini, mbinu za kivita na wameweza kufahamu matumizi sahihi ya silaha mbalimbali. Pia Askari hao wamejifunza uzalendo, hamasa ya kuipenda na kutamani kuitumikia nchi yao kwa uadilifu, utii na nidhamu, wamejengewa uwezo wa kuwa wakakamavu na jinsi ya kukabiliana na changamoto za kijamii. Pia askari 5 kati yao wameanza mafunzo ya Ulinzi na Usalama.
Katika kuitimisha hafla hiyo Mhe. Nyundo amewahadi askari wa jeshi hilo kuwapa kipaumbele katika fursa za ajira na mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya jeshi la kujenga taifa. Aidha Mhe. Nyundo ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa kuacha tabia ya kubeza wanapopata taarifa ya jambo au wito wa serikali, badala yake amewasihi wananchi kutumia muda huo kusikiliza, kutafakari na mwisho kufanya utekelezaji wa jambo husika.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa