Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa Tanzania haikusudii kusafirisha mazao ghafi kwenda nje ya nchi kwani kufanya hivyo kutasababisha kupotea kwa ajira nyingi kwa vijana nchini.
Dkt. Jafo ameyasema hayo wakati wa Maonesho ya Nane Nane 2025 Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, tarehe 8 Agosti 2025.
Amesema kuwa katika kulinda uchumi wa nchi, amefurahishwa na juhudi za vyama vya ushirika katika kuongeza thamani ya mazao kupitia kuanzisha viwanda vya ubanguaji wa korosho, hatua itakayosaidia kuondokana na usafirishaji wa mazao ghafi.
Aidha, Dkt. Jafo amewasihi wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuchukua maarifa waliyoyapata katika maonesho hayo na kuyatekeleza kwa vitendo ili kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi, hivyo kuinua uchumi wa maeneo yao na wa taifa kwa ujumla.
Vilevile, Dkt. Jafo amezipongeza taasisi za kifedha, hususan mabenki, kwa kutoa huduma za elimu na mitaji kwa wakulima, wavuvi na wafugaji, huku riba ya mikopo hiyo ikiwa chini ya asilimia 10.
Aidha, ametoa rai kwa wataalamu mbalimbali wa serikali kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wakulima na wajasiriamali, badala ya kuwa kikwazo katika shughuli zao za kiuchumi.
Pia, Dkt. Jafo ameziagiza taasisi za SIDO na TBS katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuhakikisha zinawalea na kuwaendeleza wajasiriamali ili waweze kupata maendeleo ya kiuchumi katika sekta za kilimo, uvuvi na ujasiriamali kwa ujumla.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa