Kilwa,
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iko mbioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi Nangurukuru.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa Ndg. Renatus Mchau alipokuwa akijibu swali la papo kwa papo la Diwani wa Viti Maalum Mhe. Amina Kaudunde katika kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kilichofanyika katika ukumbi wa jumba la maendeleo Mjini Kilwa Masoko Septemba 22 lililohoji ni kwani nini ujenzi wa Stendi ya Nangurukuru unachelewa licha ya fidia kutolewa kwa waliokuwa wanamiliki eneo hilo.
Akijibu swali hilo Mchau alisema kuwa Mchoro na mchakato wa kumpata Mkandarasi ili kumsainisha mkataba ndio sababu kubwa iliyopelekea kuchelewa kwa zoezi la ujenzi wa stendi hiyo.
Mchau alisema Halmashauri imejipanga kuhakikisha Mradi wa ujenzi wa Stendi hiyo unakamilika haraka iwezekananavyo ili usaidie kuiongezea Mapato Halmashauri ya wilaya ya Kilwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti napenda Kujibu swali la lililoulizwa na Mhe. Kudunde kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa Stendi ya Nangurukuru, Mhe Mwenyekiti Ujenzi wa Stendi umechelewa kidogo kuanza kwa sababu tulikua tuna hangaikia suala la mchoro na kumpata mkandarasi na kumsainisha mkataba ili anze shughuli ya ujenzi na mchakato umeenda vizuri kwahiyo tunatarajia kuanza kutekeleza Mradi huo muda wowote baada ya vitu vingine kukamlika” Alisema Mchau.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya kilwa Mhe. Abuu Mussa Mjaka amemtaka Mkurugenzi wa Halmasahuri ya Wilaya ya Kilwa kufuatilia na kutoa mrejesho katika Baraza la Madiwani juu ya umiliki wa Ukumbi wa Jumba la maendeleo pamoja na Uwanja wa Mpira wa miguu wa Mwenge (Taifa) uliopo Mjini Kilwa Masoko.
Mjaka amesema siku za karibuni kumekuwa na sinto fahamu kwa Wananchi na viongozi juu ya umiliki wa Ukumbi wa Jumba la maendeleo pamoja na Uwanja wa Mpira wa miguu wa Mwenge (Taifa) baada ya Chama cha Mapinduzi kudai kua ndiye Mmiliki wa jengo hilo pamoja na uwanja.
“Kumekuwa na maswali mengi juu ya hili jambo, nakuagiza Mkurugenzi Fuatilia jambo hili kwa umakini na tupatiwe rejesho wa nani mmiliki wa hivi vitu”
Aidha ametaka mkurugenzi kuendelea na utaratibu uliopangwa juu ya fedha zilizotelewa kiasi cha shillingi milioni Kumi kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa Mwenge (Taifa).
“Zile pesa ambazo tumezitenga kwa ajili ya uwanja wetu zitumike kama ilivyoelekezwa na hata kama itakuja kubainika kuwa ni kweli uwanja ni wa Chama cha mapinduzi ujenzi uendelee kwani sisi tunafanya kwa ajili ya Wananchi wa Kilwa” alihitimisha Mjaka.
Sanjari na ajenda mbalimbali kulifanyika uchaguzi wa Makamu mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na wenyeviti wa kamati mbalimbali ambapo Mhe. Ibrahimu Msati Diwani wa kata ya Miteja (Cuf) aliibuka kidedea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti akimbwaga Mhe Ibrahimu Likao Diwani wa Kata ya Mingumbi (Ccm). Mhe Msati alipata kura 22 kati ya 32 huku Mhe. Likao akipata kura 10.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa